Picha Kubwa: Panya akimchezea Paka. Kushoto Juu: Katuni za Tom and Jerry ambapo Panya anamchezea Paka. Kushoto Chini: Stephanie Evans akimbeba Paka wake baada ya kushindwa kufurukuta kwa Panya.
Kweli duniani kuna mambo!! Wakati wasanii maarufu Ulaya wakibuni vikatuni vya Tom and Jerry kwa mtindo wa kufikirika, kwenye bustani moja huko Reigate, Surrey nchini Uingereza kumetokea kituko kinachoweza kuitwa cha mwaka baada ya vituko hivyo sasa kutokea laivu bustanini humo hivi karibuni.
Katika hali ya kushangaza, panya mmoja alikutwa akimchezea paka kwenye nyumba ya Bibi Stephanie Evans huku paka huyo akionekana kutulia kama kamwagiwa maji au kapigwa juju. Baada ya tukio hilo, mmiliki wake alilazimika kumbatiza rasmi paka huyo jina la Tom na yule panya jasiri jina la Jerry.
Mmiliki huyo anasema, alipotoka ndani kuelekea bustanini ndipo alipomuona panya huyo akielekea alikolala paka wake. Anasema, “Nilipata mshituko na kutulia kuona nini kitatokea nikiamini kuwa panya huyo siku zake zimefika.”
Cha kushangaza ni kwamba panya huyo alizidi kusogea bila paka wake kushituka na hatimaye akafika mpaka mdomoni na kumdandia puani paka kana kwamba alikuwa akimbusu. Alidumu hapo kwa takribani sekunde kumi hivi bila madhara yoyote.
Hatimaye panya huyo baada ya kumaliza zoezi lake hilo, kama kwenye katuni za Tom and Jerry, akageuka na kuanza kuondoka zake kupitia chini ya uzio huku paka wake akimkodolea macho tu. Kutokana na mshangao huo, nikaamua kuchukua picha ya tukio zima ili niweze kuaminika ninaposimulia kituko hiki cha mwaka.
“Mpaka sasa nimeshindwa kuelewa kwanini paka wangu aligoma kabisa kunasa panya Yule na kumfanya kiweo. Hakika bado kama naota nikikumbuka tukio lile, ni kama nilikuwa natazama katuni za Tom and Jerry.”
Katuni za Tom and Jerry zimejizolea umaarufu mkubwa duniani na kujipatia mashabiki wengi tangu zilipotengenezwa kwa mara ya kwanza mwaka 1960 na wasanii William Hanna na Joseph Barbera.
Katuni hizo zinaelezea visa vya maisha ya Tom ambaye ni paka na Jerry ambaye ni panya ambaye mara zote amekuwa mjanja mjanja katika makubaliano baina yao ambayo mara zote yanaishia kwenye mapigano makali.
Mwaka 2000, mfululizo wa katuni za Tom and Jerry ulitangazwa na Jarida la TIME kwamba ndilo onesho bora zaidi la kwenye runinga.

No comments:
Post a Comment