Muamba akibebwa kwenye machela kutolewa nje baada ya kuanguka uwanjani. Kulia: Liam Stacey akitinga mahakamani kusikiliza hukumu yake jana.
Yule kijana ‘mbaguzi’ aliyechekelea ‘kifo’ cha mchezaji wa Bolton Wanderers, Fabrice Muamba hatimaye jana amekutwa na hatia na kuhukumiwa kwenda jela.
Liam Stacey, mwenye miaka 21, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Swansea anayeishi Pontypridd, Wales Kusini alikiri kosa la kuweka ujumbe kwenye mtandao wa Twitter na hivyo ameanza kutumikia kifungo cha siku 56 jela.
Ujumbe aliotuma ulipelekwa polisi na watumiaji wenzake wa mtandao huo na mwanafunzi huyo anaweza kukosa digrii yake ya baiolojia kufuatia wanafunzi wenzake kuendesha kampeni wakitaka atimuliwe chuoni hapo.
Ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa Twitter ulisomeka: “LOL [Cheka kwa Sauti]. ****Muamba. Amekufa!!!” pia umeibua malumbano mazito na kuibua hisia kali kutoka kwa wachezaji kadhaa nyota wa Ligi Kuu ya England.
Wakati akipelekwa gerezani baada ya hukumu kutolewa jana, Stacey alikumbatiwa na marafiki zake na wazazi wake
Akitoa hukumu hiyo ya kifungo, Jaji wa Wilaya John Charles alisema: “Kwa mtazamo wangu hakuna mbadala wa hukumu ya kifungo mara moja.
“Wakati Muamba alipoanguka, ‘haikuwa dunia ya wapenda soka pekee waliokuwa wakimuombea…kila mmoja alikuwa akiomba asipoteze maisha,” alisema.Mchezaji huyo wa Bolton alichungulia kaburi baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham.
Hali ya mchezaji huyo mwenye miaka 23 inaendelea vema na sasa anaweza kutembea mwenyewe na kutazama runinga, lakini bado yuko chini ya uangalizi maalumu kumuepusha na uwezekano wa kukumbana na meseji zitakazohatarisha afya yake kwenye mtandao huo wa Twitter.
Hali ya mchezaji huyo mwenye miaka 23 inaendelea vema na sasa anaweza kutembea mwenyewe na kutazama runinga, lakini bado yuko chini ya uangalizi maalumu kumuepusha na uwezekano wa kukumbana na meseji zitakazohatarisha afya yake kwenye mtandao huo wa Twitter.
Hukumu hiyo ya Stacey imeibua mijadala mizito kwenye mtandao wa Twitter.
Baadhi yao wamepongeza hukumu aliyotoa jaji kwa kusema: “Kazi nzuri, onyo kwenu wapuuzi.”
Wengine wamelaani wakisema hukumu hiyo ni kali mno kwa mwanafunzi huyo asiyekuwa na rekodi chafu ya makosa ya jinai.
Lakini Mwendesha Mashitaka wa Wales, Jim Brisbane amesema lugha yoyote ya kibaguzi ni makosa popote pale na kwenye chombo cha habari.
“Tunatarajia kesi hii itakuwa onyo kwa yeyote ambaye anadhani maoni anayotoa kwenye mtandao yanaweza kuwa juu ya sheria,” aliongeza.

No comments:
Post a Comment