Matukio mbalimbali mara baada ya Kiungo wa Bolton Wanderers kuanguka uwanjani katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham Hotspurs kwenye Uwanja wa White Hart Lane, London. Hadi mechi inavunjwa, timu hizo zilifungana bao 1-1.
EXCLUSIVE!! Mchezaji wa kiungo wa timu ya soka ya Bolton Wanderers, Fabrice Muamba ameanguka ghafla uwanjani zikiwa zimesalia dakika chache kufikia mapumziko katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham Hotspurs kwenye Uwanja wa White Hart Lane, London jana.
Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England (U-21) mwenye miaka 23 alilazimika kupatiwa huduma mbele ya mashabiki 36,000 baada ya hali yake kuwa mbaya.
Muamba mwenye mtoto wa kiume, Joshua alimvika pete ya uchumba rafiki yake wa siku nyingi, Shauna siku ya Valentine mwaka huu.
Baada ya kuanguka uwanjani, Meneja wa Bolton Owen Coyle alipiga kelele, “Ameanguka,” kabla ya kutimua mbio kuelekea aliko Muamba huku akifuatana na watu wa huduma ya kwanza.
Kisha wachezaji wa timu zote mbili wakaungana katika majonzi hayo kusubiri kujua hatima ya mchezaji huyo ambaye aliwahi kuchezea Arsenal na Birmingham.
Mchezaji huyo ambaye alizaliwa Zaire, alibebwa hadi nje ya uwanja kwenye machela huku mashabiki wakiweka mikono yao kichwani kuonyeshwa kushitushwa na tukio hilo na wengine wakiangua kilio.
Mwamuzi Howard Webb alivunja pambano baada ya tukio hilo.
Waandishi wa habari walioshuhudia tukio hilo wamesema Muamba alishindwa kupumua.
Imethibitishwa kwamba Meneja Coyle na mshambuliaji wa Bolton Kevin Davies waliambatana na Muamba kwenye gari la wagonjwa kuelekea Hospitali ya Kifua ya London iliyoko Bethnal Green, Mashariki mwa London.
Kwa mujibu wa baadhi ya taarifa, watu wa huduma ya kwanza walifaulu kumfanya Muamba aweze kupumua tena wakati wakiwa njia kuelekea hospitali.
Bolton imethibitisha baadaye kuwa mchezaji huyo ‘hali yake ni mbaya’ na amelazwa chumba cha wagonjwa wenye uangalizi maalumu kwenye hospitali ya maradhi ya moyo.
Hakukuwa na mchezaji yeyote jirani na Muamba wakati akianguka na wala hakuhusika kwenye purukushani ya kuwania mpira.
Ilitangazwa uwanjani hapo kwamba mechi imevunjwa, na mara uwanja ulilipuka kwa mayowe huku wakitaja jina la Muamba.
Mtangazaji wa ESPN, John Barnes alisema, “Kwa jinsi wachezaji wa timu zote mbili walivyolipokea ni dhahiri tukio hili zito.”
Kevin Keegan aliongeza kwa kusema, “Jermain Defoe ameonekana kuchanganyikiwa kabisa. Mashabiki wamepatwa na mshituko mkubwa sana na sijawahi kuona kitu kama hiki uwanjani hapo kabla.”
“Tunaungana na familia yake katika janga hili,” alimalizia Keegan.
Baadaye Bolton Wanderers ilitoa tamko kwenye mtandao wake, “Bolton inathibitisha kuwa Muamba amepelekwa hospitali baada ya kuanguka uwanja wa White Hart Lane jioni hii katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA. Hakuna taarifa zaidi kwa sasa.”
Mwenyekiti wa Chama cha Soka England, David Bernstein kwa niaba ya chama hicho amemtakia afya njema Muamba.
Mapema jana, Muamba kwenye mtandao wa Twitter alielezea shauku katika pambano la timu yake ya Bolton kwenye Uwanja wa White Hart Lane.

No comments:
Post a Comment