Baada ya ajali mbaya ya gari na kufariki maeneo ya Manzese Darajani, msela mmoja aliyekuwa amepanga chumba Kwa Mtogole, Dar es Salaam akafika mbinguni bwana.
Baada ya dakika kadhaa za kushangaa shangaa likasikika tangazo kwamba majina yanaanza kusomwa ili kila mmoja hapo ajue mahali pa kwenda. Kushoto kwa anayesoma majina hayo ni wale wote wanaokwenda motoni na kulia kwake ni wanaokwenda peponi.
Umati ulikuwa mkubwa mno kiasi kwamba ilikuwa vigumu sana watu kutambuana. Ndipo majina yakaanza kusomwa na watu kushika njia zao kwa kadri walivyoishi duniani.
Yakaitwa majina kama mia sita hivi ndipo msela wa Kwa Mtogole akaitwa jina lake. Kwa jinsi alivyokuwa katili na mwizi, hakusubiri kuoneshwa pa kwenda kwani alinyoosha moja kwa moja kushoto. Kama alijua, kweli msomaji alipomaliza kutaja jina lake la pili akaelekeza aelekee huko huko motoni.
Alipofika kwenye bwalo moja huko akakuta umati mara mbili ya ule aliouona pale nje. Akaanza kupepesa macho huku na kule huku akiendelea kupenya katikati ya msitu wa watu bila kukutana na yeyote anayemjua.
Baada ya dakika kama ishirini hivi, akaamua kumuuliza jamaa mmoja aliyekuwa jirani naye, “samahani naulizia kama umemuona mtu yeyote wa Manzese hapa.” Jamaa akajibu, “Ooh umepotea dogo, hiki ni kijiwe cha watu wa Tandika. Nenda kule mwisho utakuta wenzako.”
Msela akaelekea kule alikooneshwa. Mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni mchungaji wa kanisa la jirani na alikokuwa amepanga. Msela akapiga ukulele wa mshangao, “Hee, mchungaji na wewe uko huku?” Yule mchungaji akamkatisha, “Shiiiiiiii, nyamaza, Askofu yuko hapo nyuma.” Mh, kweli matendo yetu duniani ndio yatakayotuhukumu!
No comments:
Post a Comment