Wednesday, March 28, 2012

AJIPIGA KIBERITI KUPINGA ZIARA YA RAIS WA CHINA...

Sio kuigiza, Yeshi akionekana pichani anavyoteketea kwa moto wakati wa maandamano. Picha ndogo chini, Dalai Lama (kushoto) na Rais Hu Jintao (kulia).

Muandamanaji mmoja wa Tibet anatibiwa majeraha mabaya ya moto baada ya kujipiga kiberiti kwenye maandamano kupinga ziara ya Rais wa China nchini India.
Muandamanaji huyo mwanaume alikimbia mita 50 mjini New Delhi juzi huku akiwaka moto mwili mzima wakati waandamanaji wakipinga utawala wa kimabavu wa China dhidi ya Tibet.
Jamphel Yeshi alijivika ujasiri na kukimbia jirani na vipaza sauti mbele ya jengo la Bunge la India kwenye mji mkuu wa nchi hiyo.
Raia huyo wa Tibet aliungua asilimia 98 ya mwili wake na hali yake hospitalini jana ilielezwa kuwa ni mbaya sana.
Aliungua kwa takribani dakika mbili, lakini baadhi ya nguo zake zikiweza kuhimili moto huo na ngozi yake ilibadilika na kuwa kama mkaa wakati akikimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Yeshi, mwenye miaka 27, alitoroka Tibet mwaka 2006 na amekuwa akiishi New Delhi kwa miaka miwili sasa, wanaharakati wameeleza.
Alianguka baada ya mita 50 na waandamanaji wenzake kuanza kuzima moto huo kwa kutumia bendera za Tibet walizokuwa wamebeba.
Yeshi baadaye alitibiwa majeraha ya moto kwenye hospitali ya New Delhi, mmoja wa waratibu wa maandamano hayo kutoka Tibet alisema.
Ameonesha aina ya kipekee ya kuandamana wakati Rais wa China Hu Jintao akijiandaa kuwasili nchini India baadaye wiki hii kwa ajili ya kilele cha mkutano.
Zaidi ya waandamanaji 600, wakiwa wamebeba mabango na vipeperushi walipita mjini New Delhi wakielekea jengo moja jirani na jengo la Bunge la India ambako waandamanaji walipanga kufanya mkutano wao.
Baadhi yao walibeba vipeperushi vikisema, ‘Tibet inateketea’ na ‘Tibet sio sehemu ya China’.
Kwenye eneo la maadamano hayo, bango kubwa lilionesha sura ya Rais wa China akiwa anachuruzika damu na maandishi yaliyosomeka, ‘Hu Jin Tao hakaribishwi’ kwenye kilele cha mkutano.
Wakati vipaza sauti zikiutangazia umati uliokusanyika hapo, ndipo muandamanaji huyo alipojipiga kiberiti na kukatiza katikati ya eneo hilo huku akikimbia kwa kasi.
Baada ya kushuhudia mtu akijichoma moto mwenyewe, mmoja wa walioona tukio hilo alisema, ‘Hiki ndicho wanachokikabili China vinginevyo waipatie uhuru Tibet.’
Takribani watu 30 wa Tibet wamejichoma moto miaka kadha iliyopita kupinga China kuikalia kimabavu ardhi yao.
Kiongozi wa Tibet, Dalai Lama amekuwa akiishutumu China kwa sera zake za kibabe na kibinafsi.
China imesema Tibet siku zote imekuwa sehemu ya mipaka yake. Watibet wamekuwa wakisema eneo la Himalaya limekuwa huru kwa karne nyingi sasa.

1 comment:

Anonymous said...

Dah, huyu jamaa kiboko.