Richard Norris alivyokuwa kabla na baada ya tukio (picha ya chini). Picha kubwa ni madaktari wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Mwanaume mwenye miaka 37 aliyejijeruhi vibaya kwa bunduki mwaka 1997 amepatiwa sura mpya, meno, ulimi na taya katika kile madaktari walichokiita upasuaji mgumu kabisa wa upandikizaji sura mpya kuwahi kufanyika.
Maofisa kutoka kituo cha tiba cha Chuo Kikuu cha Maryland wametangaza juzi kuwa Richard Lee Norris anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji uliochukua saa 36 wiki iliyopita.
Ameanza kupata hisia kwenye uso wake na tayari ameanza kupiga mswaki na hata kunyoa ndevu.
Pia ameanza kuhisi harufu, kitu ambacho alikuwa akishindwa kufanya mara baada ya ajali hiyo.
Kwa miaka 15, Norris amekuwa akiishi kwa shida huku akificha uso wake kwa kuvaa kinyago na kutoka nje nyakati za usiku tu.
Upandikizaji huo utamrejeshea hamu ya kuishi, amesema Dk. Eduardo Rodriguez, kiongozi wa jopo la madaktari waliofanya zoezi hilo la upasuaji.
“Inashangaza unapomuangalia. Ni vigumu kuamini.
“Kabla, watu walikuwa wakimshangaa Norris sababu amevaa kinyago na walikuwa na hamu ya kuona anachoficha,” anasema Rodriguez.
“Sasa, wana sababu nyingine ya kumshangaa, na hakika inashangaza.”
Wapasuaji wanaita ni upandikizaji sura endelevu duniani ambao umemuwezesha mwanaume huyo wa Virginia kuvua kinyago baada ya miaka 15 na kutembea kwa kujiamini.
Wakati alipojipiga risasi mwenyewe usoni mwaka 1997, aling’oa pua yake, midomo na kila kitu mdomoni mwake. Alilazimika kupata jitihada za ziada kuokoa maisha yake, lakini hakuna iliyofanikiwa kama hii ya sasa.
Alipatiwa sura mpya kutoka kwa mchangiaji asiyefahamika wiki iliyopita ambaye viungo vyake vimesaidia maisha ya wagonjwa wengine watano siku hiyohiyo.
Siku sita baada ya upasuaji huo, anaweza kuchezesha ulimi wake, kufumba na kufumbua macho na afya yake inaimarika kwa kasi kuliko madaktari walivyotarajia.
“Hakika kwa sasa anajitazama kwenye kioo akinyoa na kupiga mswaki meno yake, jambo ambalo hatukulitegemea,” anasema Dk. Eduardo Rodriguez, Profesa Shule ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Maryland na kiongozi wa jopo la madaktari waliofanya upasuaji huyo, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Wakati Norris alipofungua macho yake siku ya tatu baada ya upasuaji huku familia yake ikiwa imemzunguka kitandani, alitaka ajitazame kwenye kioo.
“Akaweka kioo chini na kunishukuru huku akinikumbatia,” anasema Dk. Rodriguez.
Upandikizaji sura kwa Norris unaonekana kuwa ni wa mafanikio zaidi kwa sasa kufuatia picha na video zilizosambazwa kwa vyombo vya habari katika mkutano huo. Anaendelea kupata nafuu na bado yuko hospitalini hivyo hakuweza kuhudhuria mkutano huo.
Kuhakikisha Norris anafanya shughuli zote kama kawaida, madaktari wamempatia ulimi utakaomuwezesha kutamka maneno, kula na kumung’unya, mpangilio sahihi wa meno, na kuunganisha mishipa yake ya fahamu itakayomuwezesha kutabasamu.
Upandikizaji sura kwa Norris umekuwa wenye mafanikio zaidi kuwahi kutokea kwenye miji ya Forth Worth, Texas na Boston, Massachusetts mwaka jana.
Amekuwa wa kwanza kufanyiwa upandikizaji wa sura nzima katika Marekani na kuweza kuendelea kuona bila matatizo.
Operesheni ya kwanza ya kupandikiza sura nzima ulifanyika Ufaransa mwaka 2005 kwa mwanamke aliyeng’atwa na mbwa wake. Kliniki ya Cleverland ilifanya upandikizaji sura nzima wa kwanza katika Marekani mwaka 2008.
Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo imekuwa ikifadhili sura na upasuaji mikono wenye lengo la kusaidia wanajeshi wake wanaojeruhiwa vitani.
Zaidi ya askari 1,000 wamepoteza mkono au mguu nchini Afghanistan ama Irak, na serikali inakadiria zaidi ya askari 200 watalazimika kupandikiziwa sura.

No comments:
Post a Comment