MWANAMKE ANYONGWA KWA KHANGA NA KUTELEKEZWA MUSOMA...

Kamanda Absalom Mwakyoma.
Mwanamke ambaye jina lake halikufahamika mara moja mkazi wa Buhare Mgaranjabo, mjini Musoma, amekutwa amekufa kwa kunyongwa na khanga na mwili wake kutupwa kichakani na watu wasiojulikana huku nguo zake za ndani zikiwa zimechanwa. 
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma ilisema tukio hilo lilitokea Januari 31 saa 10.15 jioni.
Ilisema kando ya mwili wa marehemu zilikutwa nguo za ndani zikiwa zimechanwa na  dumu la kuchotea maji likiwa meta 20 kutoka ulipokuwa mwili.
Inadaiwa kuwa nywele zake zilikutwa zimefungwa kwenye kijiti kichakani hapo na khanga ikiwa shingoni huku ulimi ukiwa umechomoza nje.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini waliofanya tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake. Kuna taarifa kuwa marehemu ameacha mtoto wa umri wa miezi mitatu.
Kamanda Mwakyoma alitoa mwito kwa wananchi watakaokuwa na taarifa za watu au mtu aliyehusika na mauaji hayo wazitoe kwa siri kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Matukio ya mauaji yamekuwa kero kwa wananchi wa mkoa wa Mara ambapo wilaya ya Butiama inaongoza kwa mauaji ya kikatili ambapo jumla ya watu wanne waliuawa katika kipindi cha Novemba mwaka jana hadi Januari.

No comments: