HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MKUTANO WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA, SAMIA SULUHU HASSAN NA MABALOZI WA TANZANIA NJE YA NCHI UTAKAOFANYIKA ZANZIBAR KUANZIA TAREHE 14 HADI 21 NOVEMBA 2022

 

HOTUBA YA DKT. STERGOMENA TAX (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MKUTANO WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA, SAMIA SULUHU HASSAN NA MABALOZI WA TANZANIA NJE YA NCHI UTAKAOFANYIKA ZANZIBAR KUANZIA TAREHE 14 HADI 21 NOVEMBA 2022

 

 

Ndugu Wahariri;

Ndugu wanahabari;

Mabibi na Mabwana;

 

Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Ndugu wahariri, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana siku ya leo tukiwa na afya njema.

Pili, nawashukuru kwa kuitikia wito wetu na kuweza kuhudhuria mkutano huu. Pia, nawashukuru na kuwapongeza kwa ushirikiano mnaoutoa kwa Wizara na kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya kuuhabarisha Umma kuhusu umuhimu na mchango wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika maendeleo ya Taifa letu.

Ndugu wahariri, nimewaita hapa leo katika mkutano huu ambao ni wa kwanza tangu niteuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mwezi Oktoba 2022.

Natambua kwa nyakati tofauti katika nafasi nyingine niliziwahi kushika tulikutana na kufanya kazi pamoja na kwa ushirikiano mkubwa. Nashukuru ushiriki wenu leo inanipa nafasi nyingine ya kufahamiana nanyi. Ni imani yangu kuwa mtaendelea kunipa ushirikiano mzuri katika utekelezaji wa majukumu yangu haya mapya kama mlivyokuwa mkinipa katika nafasi nyingine nilizowahi kushika huko nyuma.

Wote mnatambua ukubwa na unyeti wa Wizara hii na kazi kubwa ambayo Wizara inayo ya kusimamia na kukuza ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine, mashirika ya kikanda na kimataifa na majukumu mengine yakiwemo kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita pamoja na mambo mengine kwenye diplomasia ya uchumi. Hivyo ili majukumu yetu yaeleweke vyema kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa, mchango wenu unahitajika kwa kiasi kikubwa.

Aidha, tunatambua kuwa, ili vyombo vyenu viweze kutekeleza vyema majukumu haya ya kuhabarisha kuhusu masuala ya diplomasia, mafunzo mahsusi ya mara kwa mara kwa wanahabari yanahitajika. Ni matumaini yangu kuwa mafunzo kuhusu namna bora ya kuandika taarifa za kidiplomasia yaliyoandaliwa na Wizara na kufanyika Dar Es Salaam mwezi Julai 2022 yalikuwa na tija kubwa kwa wale waliopata fursa ya kushiriki.

Mwezi huo huo pia, Wizara kwa kushirikiana na GIZ ilitoa mafunzo kuhusu mtangamano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo yalifanyika Bagamoyo kwa siku tatu. Nawaahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na nyinyi kuandaa mafunzo kama hayo kadri hali itakavyoruhusu ili kuongezeana ujuzi utakaokidhi mabadiliko yanayotokea duniani hivi sasa.

Ndugu wahariri, baada ya utangulizi huo mfupi kwenu, naomba sasa niwafahamishe kuhusu Mkutano baina ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi.

Mkutano huo umepangwa kufanyika mjini Zanzibar kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022. Mkutano huo ambao ni wa kwanza baina ya Mheshimiwa Rais na Mabalozi tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani, unabeba Kaulimbiu ya Mwelekeo Mpya Katika Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi”.

Ndugu Wahariri, Lengo la Mkutano huu ni kutoa fursa kwa Waheshimiwa Mabalozi na watendaji wa Wizara wanaoshiriki katika uratibu wa utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje kupokea maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine kuhusu mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi, kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi, kuainisha changamoto katika utekelezaji wa majukumu na kuja na mikakati madhubuti ya namna ya kuzitatua changamoto mbalimbali za kiutendaji, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Aidha, Mkutano huu ni fursa kwa Tanzania kuandaa mikakati ya pamoja ya namna ya kujiweka sawa (repositioning) ili kuhakikisha Taifa linanufaika ipasavyo kutokana na fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo ya uwakilishi.

Ndugu wahariri, Wizara itatoa mialiko kwa vyombo vya habari kushiriki mkutano huu wakati katika nyakati tofauti kama ifuatavyo;

1.    Tarehe 14 Novemba, 2022, nitafungua kikao cha Waheshimiwa Mabalozi, Konseli Wakuu na Menejimenti ya Wizara ambacho kitafanyika mpaka tarehe 17 Novemba, 2022. Katika siku hizo tumealika wadau mbalimbali wa Sekta ya umma na binafsi kuongea na waheshimiwa Mabalozi masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu yao

2.    Tarehe 17 Novemba, 2022 Waheshimiwa Mabalozi na Menejimenti ya Wizara watatembelea vivutio vya utalii na miradi ya maendeleo ya kimkakati Zanzibar ikiwa ni pamoja na Bandari ya Malindi na Manga Pwani;

3.    Tarehe 18 Novemba, 2022 kutakuwa na Mkutano kati ya Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na waheshimiwa Mabalozi na Menejimenti ya Wizara; na

4.    Tarehe 19 Novemba, 2022 kutakuwa na Mkutano kati ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mabalozi na Menejimenti ya Wizara.

Ndugu Wahariri, nichukue fursa hii kuvialika vyombo vyenu kushiriki katika matukio haya na kuwaomba muupe mkutano huu umuhimu na nafasi ya kipekee katika vyombo vyenu ili umma wa Watanzania na dunia kwa ujumla uweze kufahamu mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje.

Aidha, Waheshimiwa Mabalozi wetu wote kutoka Balozi zote 45 wanaoiwakilisha nchi yetu nje ya nchi watakuwepo nchini na moja ya majukumu waliyoelekezwa ya kufanya wakiwa hapa nchini ni kujulisha umma kuhusu utekelezaji wa majukumu yao. Hivyo, niwaombe kwa niaba yao mtoe ushirikiano watakapohitaji fursa kwenye vyombo vyenu.

Ndugu wahariri, kama nilivyodokeza awali kuwa, mkutano huu una lengo la kuweka mikakati ya kuboresha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ili ilete tija zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Baada ya mkutano huu Balozi zetu zitajipanga upya ili kuongeza ubunifu katika kuiletea nchi maendeleo ili kufikia azma ya Serikali ya Dira ya Maendeleo ya 2025.  

Hadi ninavyoongea na nyinyi, Balozi zimefanya kazi nzuri na ya kuridhisha ya kutafuta wawekezaji, masoko ya bidhaa zetu, misaada na mikopo nafuu ya maendeleo na kuvutia watalii wengi kuja nchini. Mfano mzuri wa hivi karibuni ni ziara za viongozi wetu wakuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini China, ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango nchini Ivory Coast, ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi nchini Oman na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) nchini Jamhuri ya Korea.

Ziara hizo zimeratibiwa vizuri na Balozi zetu na zimekuwa na mafanikio makubwa katika diplomasia ya Tanzania.

Ndugu wahariri, baada ya kusema hayo, naomba kuwashukuru sana kwa kuitikia wito wetu wa kushiriki kwenye Mkutano huu.

 

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

 

No comments: