Kaya 2,857 wilayani Kilosa zimekosa makazi kutokana na
nyumba 379 kubomoka na nyingine 997 kuzingirwa na maji yaliyotokana na mafuriko
yaliyokumba wilaya hiyo ya Mkoa wa Morogoro.
Mafuriko hayo yametokana na mvua kubwa zilizonyesha katika safu za milima ya Wilaya za Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma na maji yake kujaa mto Mkondoa unaokatisha katika mji wa Kilosa.
Mkuu
wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele alisema
hatua za awali ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuhifadhi kwa muda
waathirika wa mafuriko kwenye shule ya
Msingi ya Lamlilo, mahakama ya mwanzo na katika ofisi ya mtendaji kata ya
Magomeni.
Aidha
alisema, mahitaji ya awali kwa waathirika hao yameshaandaliwa yakihusisha
chakula, maji, dawa wakiwa eneo hilo kwa
muda wakisubiri kuhamishiwa katika
kambi maalumu zitakazotengwa.
Alitoa
taarifa hiyo juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe aliyekwenda
kukagua maeneo yaliyoathiriwa.
Henjewele
alisema mafuriko hayo yalitokea usiku wa kuamkia Januari 5, pia yameathiri
miundombinu ya barabara ya Kilosa – Mikumi
ambayo kwa sasa haipitiki. Pia
imeharibu mashamba huku kata ya Magomeni
ikitajwa kuathirika zaidi.
Pia
nyumba 33 zilizopo katika Kata ya Berega
mapaa ya majengo ikiwemo vyoo vya shule za Msingi Kiegeya, Mugugu na Berega,
yameezuliwa.
Diwani
wa Kata ya Magomeni, Abdallah Huwel alishauri serikali kujenga tuta upande wa pili wa mto Mkondoa.
Kumbukumbu zinaonesha mafuriko makubwa yalitokea mwaka 1964 na 1978, 1997; Desemba 2009 na kuendelea hadi Januari, 2010
na kusababisha vifo vya watu wawili. Uliathiri watu 23,980 sawa na kaya
5, 605.
No comments:
Post a Comment