Afya ya Kardinali Pengo yaimarika

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete anaendelea vizuri na anaweza kuruhusiwa wiki ijayo.


Pengo amelazwa katika taasisi hiyo iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kuanzia usiku wa Desemba 31, mwaka jana na ametolewa katika chumba cha uangalizi maalumu na kuwekwa katika wadi ya kawaida.  
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Mohamed Janabi, alisema afya ya Pengo inaendelea vizuri na kwamba endapo hali ikiendelea hivyo anaweza kuruhusiwa kutoka hospitali wiki ijayo.
Kuhusu ugonjwa unaomsumbua, Janabi alisema kwa mujibu wa taaluma yao hawana sababu ya kuzungumzia ugonjwa wake labda mwenyewe akipona anaweza kuelezea ugonjwa uliokuwa ukimsumbua. Juzi, Rais John  Magufuli  akiongozana na mkewe, Janeth  Magufuli walimtembelea Pengo ili kumjulia hali, kumpa pole na kumuombea afya njema ili aweze kuendelea na shughuli zake za kutoa huduma za kiroho kwa wananchi.

No comments: