Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
linawashikilia vijana watano wa kundi la wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) kwa tuhuma za kufanya uchochezi na kufanya mikusanyiko isiyo halali
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema vijana hao
wamekamatwa kwa nyakati tofauti kwa makosa ya kuunda kikundi kisicho halali kwa
mujibu wa sheria za nchi na kuwahamasisha wenzao, kuandamana hadi Ikulu kwa
Rais Jakaya Kikwete kudai ajira za kudumu.
“Tunawashikilia vijana watano ambao ndio
viongozi wa kikundi kinachojiita umoja wa wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa.
Mwenyekiti ndio alikuwa wa kwanza kukamatwa na wengine tuliwakamata juzi mara
baada ya kukusanyika eneo la Msimbazi Centre na Muhimbili,” alisema Kova.
Akieleza chanzo cha vijana hao kutaka
kuandamana kuelekea Ikulu, alidai wahitimu hao wanadai kuahidiwa ajira za
kudumu walipomaliza mafunzo yao na hivyo baada ya kukaa kwa muda mrefu bila
kuajiriwa, ndipo wakaamua kuanzisha kikundi hicho ili kwenda kumwona Rais Kikwete kumweleza tatizo la ajira
linalowakabili.
“Vijana hawa wanadai kuwa waliahidiwa kupewa
ajira za kudumu mara baada ya kumaliza mafunzo yao ya JKT. Jambo hili sio la
kweli, kwani tumefanya uchunguzi na kubaini hakuna mkataba wowote unaosema
wakimaliza mafunzo lazima waajiriwe, bali kila mtu anatakiwa kutumia ujuzi
alioupata kujiajiri. Lakini walipokaa
kwa muda mrefu bila kuona ahadi yao
inatekelezwa, wakaamua kuanzisha kikundi chao ambacho sio halali kwa mujibu wa
sheria za nchi.
Hadi sasa tumeandaa jalada la mashitaka na
tumelikabidhi kwa mwanasheria wa serikali kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani
watuhumiwa hawa kujibu mashitaka yanayowakabili,” aliongeza Kova katika taarifa
yake.
Alitaja vijana wanaoshikiliwa na Polisi kuwa
ni Mwenyekiti wa kikundi hicho George Mgoba (28) mkazi wa Mabibo Loyola, Katibu
wao Linus Emmanuel (28) mkazi wa Tabata, Emmanuel Richard (28) mkazi wa Kawe,
Jacob Joseph (36) mkazi wa Mabibo na Rizione Ngowi (27) mkazi wa Mtoni
Mtongani.
Akizungumzia tuhuma za kutekwa na kuteswa kwa
George Mgoba, Kova alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini
tukio hilo kama ni la kweli na kwanini watu hao walimteka.
“Tunaendelea na uchunguzi kubaini kama ni
kweli kijana huyo alitekwa kama anavyodai kuwa Februari 16 alitekwa na
kupatikana tarehe 19 majira ya saa nne
usiku huko Tungi Kibaha kandokando ya barabara, pia tujue ni akina nani
walimteka na kwasababu zipi kisha watu hao tutawapeleka mahakamani,” alisema
Kova.
Kova alieleza kuwa “Februari 22 mwaka huu
majira ya saa kumi na moja jioni, George Mgoba alijaribu kutoroka wadini katika
Hospitali ya Muhimbili lakini polisi walibaini ujanja wake na kufanikiwa
kumweka kizuizini. Lengo lake ilikuwa ni kukimbia matibabu na kuzua hofu kwa
wananchi”.
Kwa sasa Mwenyekiti huyo wa vijana hao bado
amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, akipatiwa matibabu. Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na
Huduma kwa Wateja katika Hospitali hiyo ya
Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema
jana kuwa hali ya mtu huyo, inaendelea vizuri na afya yake imeimarika.
Wakati huo huo, katika taarifa yake kwa vyombo
vya habari baadaye jana, Kova alimtaka Makamu Mwenyekiti wa Vijana hao, Parali
Kiwango (25) mkazi wa Temeke Mikoroshini ajisalimishe mara moja Polisi kwa
ajili ya mahojiano zaidi, kabla jeshi hilo halijaanza kumtafuta.
“Jeshi la Polisi linamtaka Makamu Mwenyekiti
ajisalimishe mara moja kwani jana alipoona Katibu wake amekamatwa alikimbia na
kutokomea kusikojulikana. Yeye kama ni mhitimu wa JKT hatakiwi kukimbia, bali
ajisalimishe mwenyewe katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam au kituo chochote cha
Polisi kilicho karibu na alipo,” aliongeza Kova.

No comments:
Post a Comment