Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza tani saba za
juisi ya U-Fresh inayozalishwa na Kiwanda cha U-Fresh Food Limited ya Tegeta, Dar es Salaam kwa
sababu ya kukosa viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Juisi hizo, ambazo ni katoni 1,400, ziliteketezwa katika
dampo la Pugu, nje kidogo ya Dar es Salaam, kwa gharama za wamiliki wa kiwanda
hicho, ambao ni raia wa China. Katoni moja inauzwa Sh 4,000.
Akizungumza wakati wa uteketezaji wa juisi hizo
ulioshuhudiwa na Mkaguzi wa Viwango vya Bidhaa wa TBS, Inspekta Edimitha
Protace, Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano cha shirika hilo, Roida Andusamile
alisema, tani hizo za juisi zilizoteketezwa zimekusanywa na mzalishaji mwenyewe
kutoka sokoni.
"Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdalla Kigoda,
aliwaagiza wazalishaji wote waliozuiwa kuendeleza uzalishaji nchini kwa sababu
bidhaa zao hazikidhi matakwa ya viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa,
waziondoe sokoni ndani ya siku 14 zilizoanza Januari 28 na kuisha kesho
(leo)".
"Kwa asilimia kubwa, wazalishaji hao wametekeleza agizo
la Waziri, na sisi kama shirika tunajipanga kuingia sokoni kufanya ukaguzi wa
siri, kuhakikisha endapo zimeondolewa zote kutoka katika masoko mbalimbali
nchini, kwa sababu tuna orodha ya wazalishaji hao. Lengo letu ni kujiridhisha
kuwa walaji wanapata bidhaa bora na si bora bidhaa," Andusamile
alisema.
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa U-Fresh, Kephas Gembe
alisema, wanakiri kuwa juisi yao haikuwa bora na kwamba maelekezo yote
waliyopewa na TBS kwa ajili ya kurekebisha kasoro zilizoonekana wameyatekeleza
na kuliomba shirika hilo liwakague upya ili waendeleze uzalishaji.
Kwa mujibu wa Gembe, kuanzia Desemba 24, mwaka jana,
walipozuiwa kuendeleza uzalishaji walikuwa wakiwasiliana na wateja wao ili wasimamishe
uuzaji.
"Hata tangazo la waziri lilipotolewa tayari tulikuwa
tumeanza kuzikusanya. Jana pia (juzi) tuliutangazia umma utuletee taarifa ya
wanaoendelea kuziuza ili tukaziondoe madukani mwao. Wauzaji ambao hatujawafikia
kuzichukua nao tumewaomba wazirudishe kiwandani ili tufanye utaratibu wa
kuziteketeza," alisema.
Akijibu ni kwa nini zilizofikishwa dampo ili kuteketezwa
zilikuwa kidogo zaidi ya zilizokutwa kiwandani wakati wa ukaguzi wa kushtukiza,
Meneja Masoko huyo alisema, kiasi hicho ndicho kilichokusanywa kutoka sokoni na
kwamba zilizofungiwa kiwandani na TBS hazijateketezwa,kwa sababu hawana ruhusa
ya kuzigusa hadi shirika hilo lisimamie utoaji wake kujiridhisha kuwa zipo kama
zilivyokuwa zimefungiwa.

No comments:
Post a Comment