SHULE ZA VIPAJI ZASHINDWA KUFURUKUTA KIDATO CHA NNE


Shule za sekondari za Serikali zinazochukua watoto wenye  vipaji, zimeshindwa kung'aa kwenye matokeo ya kidato cha nne 2014 huku shule ya Ilboru ya mjini Arusha ikiwa ni shule ya kwanza ya Serikali na iko nafasi ya 35 kati ya shule 2,320 zilizofanya mtihani  wa kidato cha nne 2014.

Mwaka 2013, Ilboru ilishika nafasi ya 41 chini ya shule nyingine yenye vipaji ya Mzumbe ambayo katika matokeo ya sasa imeshika nafasi ya 56 na kushika nafasi ya pili katika shule za Serikali.
Wanafunzi 94 wa Ilboru walijisajili kwa ajili ya mtihani huo, huku watahiniwa 90 wakifaulu (distinction, merit, credit na pass) na wanafunzi watatu wakifeli. Ilboru ina wastani wa pointi GPA 3.74.
Mzumbe iliyoporomoka kwa nafasi 16 ukilinganisha na mwaka 2013, wanafunzi watahiniwa 110 wamefaulu na mmoja akifeli na ina GPA 3.47.
Msalato ambayo mwaka 2013 ilishika nafasi ya 63, imeshika nafasi 71 ikiwa na GPA 3.30 huku watahiniwa 85 wamefaulu. Mwaka 2013 shule hiyo ilishika nafasi ya 65.
Kibaha ikiwa miongoni mwa shule za vipaji imeporomoka nafasi 43, ikishika nafasi ya 87 baada ya kupata GPA 3.22, ambapo watahiniwa 98 wakifaulu na wanne kufeli. Mwaka 2013, shule hiyo ilikuwa nafasi ya 44.
Shule ya wavulana ya Tabora imeporomoka kwa nafasi 37 ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2013. Shule hiyo imeshika nafasi ya 93 ikiwa na GPA 3.18 ambapo wanafunzi 96 wakifaulu na wanne wakifeli. Mwaka 2013 ilikuwa nafasi ya 56.
Kilakala ambayo mwaka jana ilikuwa nafasi ya 63, imeshuka hadi nafasi ya 96 ikiwa na GPA ya 3.13, huku wanafunzi 80 wakifaulu na wanafunzi watatu wakifeli mtihani huo.
Katika kundi la shule zenye vipaji, shule ya wasichana ya Tabora ambayo matokeo yaliyopita (2013) ilishika nafasi ya 147 zimezidi kuporomoka na kushika nafasi ya 295 ikiwa na GPA ya 2.24. Wanafunzi 57 wamefaulu na watano wakifeli.
Kwa upande wa shule kongwe za jijini Dar es Salaam Jangwani imeporomoka kutoka nafasi ya 226 mwaka 2013 hadi kufikia nafasi ya 243 ikiwa na GPA 2.42, Azania iko nafasi ya 427, Zanaki (270), Bwiru (234) na Pugu (420).

No comments: