Kutokana
na wahalifu waliopambana jana na polisi na Jeshi la Wananchi (JWTZ)
kutokamatwa, hali ya wasiwasi imeendelea miongoni mwa wakazi wa mjini hapa.
Sasa
wananchi hao wameiomba Polisi kutoa tamko, kuhusu kikundi kilichorushiana
risasi na askari Polisi na kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja.
Aidha,
wananchi hao wameitaka Polisi kutoa
ufafanuzi kuhusu mwendelezo wa matukio mengi ya uhalifu wa kutumia silaha, ambayo
bado hayajapatiwa ufumbuzi, ikiwemo kutokamatwa kwa watuhumiwa wa matukio hayo.
Hata
hivyo, Msemaji wa Polisi, Advera, alisema Jeshi lake halina taarifa zaidi ya
iliyotolewa juzi na Mkuu wa Opersheni wa jeshi hilo, Kamishna Paul Chagonja.
Habari
za kipolisi zinasema kwamba bado wanaendelea kusaka wahalifu hao huku baadhi ya
vikosi vya ulinzi na usalama, vimeongezwa kwa ajili ya kupambana na wahalifu
hao.
Juzi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na
Polisi walipambana na kundi la wahalifu katika maeneo ya mapango ya Amboni na
kusababisha wanajeshi wanne na polisi wawili kujeruhiwa. Hata hivyo, kuna
habari kuwa majeruhi mmoja ambaye ni
mwanajeshi alifariki baadaye akiwa hospitalini.
Habari
zingine zinasema kwamba majeruhi wengine ambao ni polisi wanne na mwanajeshi
mmoja, wanaendelea vizuri. Kuhusu mwanajeshi aliyekufa, polisi wamegoma
kuzungumzia suala hilo, lakini habari zinasema aliyekufa ni mwanajeshi mwenye
cheo cha sajenti.
Wananchi
wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti jana, walipozungumzia tukio la juzi,
lililosababisha mapigano ya kurushiana risasi baina ya askari na wahalifu, wanaodaiwa kuficha silaha katika eneo la
Mapango ya Amboni, nje kidogo ya mji wa
Tanga.
Walisema
mpaka sasa bado hawajaridhishwa na mwenendo wa utendaji wa Jeshi la Polisi
mkoani hapa, pamoja na taarifa hafifu wanazotoa, kuhusu namna walivyoshughulikia
tukio hilo la juzi kwenye mapango hayo
ya Amboni.
Ibrahim
Mshote, mkazi wa Ngamiani Kati, alisema mbali na tukio la juzi, yapo matukio
mengine yakiwamo yaliyosababisha mauaji kwa raia, ambao walivamiwa na kuporwa
mali na watuhumiwa kushindwa kupatikana. Alisema hakuna taarifa za mwendelezo wa kushughulikiwa
kwa matukio hayo.
“Kwa
mfano kuna wananchi walilipuliwa na bomu
la kutupwa kwa mkono wakati wakitazama mpira kwenye kibanda cha video hapo
Amboni… pia yupo mfanyabiashara wa eneo la Mkumbara wilayani Korogwe ambaye
hivi karibuni alivamiwa na kuuawa kwa risasi kabla ya kuporwa mali, pia tukio
la utekaji wa gari eneo la Michungwani wilayani Handeni baada ya kuwekewa
magogo barabarani”, alisema.
Aliongeza
“Katika matukio kama hayo, tunaambiwa tu wahalifu hawakupatikana, upelelezi
unaendelea, lakini ni zaidi ya wiki mbili sasa hakuna taarifa zozote
zinazoonesha juhudi za mwendelezo wa kudhibiti wahalifu kama hao, badala yake
matukio yameendelea kuongezeka”.
Miriam
Jonas, mkazi wa Barabara ya Tano jijini Tanga, alisema kitendo cha askari
kunyang’anywa silaha mbili za SMG zenye risasi 60 kwenye kibanda cha chipsi ni
fedheha kwa kuwa vitendo hivyo vilishasahaulika mkoani hapa.
“Tulitarajia wahusika wangekamatwa ndani ya
muda mfupi, lakini wapi, Polisi hapa Tanga imeshindwa kabisa kutoa taarifa
kuhusu tukio hilo hadi Kamishna Chagonja alipokuja na kuzungumzia tukio la
juzi”, alisema.
Aidha,
Mrisho Mashaka mkazi wa Kwaminchi alisema licha ya Chagonja kuwataka wakazi wa
jiji la Tanga kutulia, kwakuwa hali ya usalama imeimarishwa, bado baadhi ya
wananchi wanayo shaka na hofu kubwa kuhusu tamko hilo.
“Kinachoendelea
kutupa hofu ni mgongano wa kauli za polisi kama tulivyosikia
kwenye
vyombo vya habari kwamba waliarifiwa kwamba silaha za moto zikiwemo walizoporwa
askari Januari 26 zimefichwa ndani ya mapango, lakini kilichokutwa ni silaha za
jadi yakiwemo mapanga, pinde na mishale na vifaa vya kutengeneza milipuko”,
alidai.
Alisema
vifaa vilivyotajwa kukutwa kwenye eneo la tukio ni tofauti na madhara waliyopata askari, waliokuwa kwenye
operesheni hiyo ya kusaka silaha hizo, ambayo yamesababisha kifo na majeraha
makubwa kwa baadhi yao, ambao sasa wamelazwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Bombo.
“Binafsi
bado napata kigugumizi kuelewa taarifa hii kwasababu bado inayo maswali mengi
ya kujiuliza, je hao ni watu wa namna gani ambao wamefanikiwa kujeruhi vibaya
askari na kisha kutoroka na silaha zilizokuwa zikitafutwa, wameelekea wapi? Je
sisi tuko salama?”,alihoji.
Walidai
vipo viashiria vinavyoonesha kwamba hali ya ulinzi na usalama mkoani hapa,
haijatengemaa kutokana na hali ya mazingira iliyobainisha kwamba wahalifu hao
waliweka makazi ndani ya mapango hayo bila kubainika mapema.
Mbali
ya silaha za jadi, vitu vingine vilivyokutwa ndani ya mapango hayo ni pikipiki mbili,
baiskeli tatu, mavazi ya aina mbalimbali na vyakula, ambavyo ni dhahiri
vinaashiria kwamba watu hao walikuwa wakijipenyeza ndani ya jamii kutafuta
huduma muhimu bila kufahamika kwamba ni wahalifu.
Aidha,
walisema ripoti ya hivi karibuni ya hali ya uhalifu mkoani Tanga, ambayo
ilitolewa na Kamanda mwishoni mwa mwaka
jana ilibainisha kuongezeka kwa makosa ya uhalifu, yanayofanywa dhidi ya
binadamu kwa asilimia 2.11, ikilinganishwa na takwimu za makosa kama hayo yaliyoripotiwa
mwaka 2013.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai alibainisha hayo wakati akitoa taarifa
kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya ulinzi na usalama mkoani humo kwa kipindi
cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba mwaka jana.
Kamanda
alisema kwamba mwaka 2014, makosa 7, 970 ndiyo yaliripotiwa kwenye vituo
mbalimbali vya Polisi wilayani, ikilinganishwa na makosa 7,805 yaliyoripotiwa
katika kipindi kama hicho mwaka 2013.
Wakazi
hao wa Tanga walidai wanaamini kwamba takwimu hizo ni kiashiria tosha kwamba
mambo hayako sawa, licha ya Kamishna Chagonja
kujitahidi kutoa matumaini.
Kutokana
na mambo kama hayo, walisema kuna umuhimu mkubwa kwa jeshi hilo kujipanga
kimkakati ili kuondoa tatizo hilo haraka kwasababu kila siku matukio mapya
yanaibuka na watuhumiwa hawapatikani.

No comments:
Post a Comment