Mabingwa wa
soka wa Tanzania Bara, Azam FC jioni ya leo wameanza vyema kampeni yao ya
kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuizima El Merreikh ya Sudan
kwa mabao 2-0.
Mbele ya
maelfu ya mashabiki wa soka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo
ya Jiji la Dar es Salaam, Azam FC iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya
tisa likifungwa na Didier Kavumbagu.
Mshambuliaji
huyu wa kimataifa wa Burundi alifunga bao la kwanza baada ya kutumia makosa ya
mabeki wa klabu hiyo ya Khartoum na kipa wao, Magoola Salum, raia wa Uganda,
ambaye mpira uliogonga miguu na kisha ukarudi tena kumgonga beki wake mmoja kabla
ya Kavumbagu kuujaza wavuni.
Akitokea
benchi, John Bocco alifunga bao la pili katika dakika ya 78 akiunganisha kwa
kichwa kona ya nahodha Salum Abubakar. Huo ulikuwa mpira wa kwanza kuugusa
Bocco uwanjani tangu aingie kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwingine, Kipre
Tchetche wa Ivory Coast.
Kwa matokeo hayo
dhidi ya moja ya timu mahiri Afrika, Azam FC inahitaji sare ya aina yoyote au
ushindi ili kusonga mbele katika michuano hiyo inayoshiriki kwa mara ya kwanza
baada ya kuwa bingwa wa Bara msimu wa 2013/2014.
Ushindi wake
umekuja siku moja baada ya wawakilishi wengine wa Tanzania Bara, Yanga
kuishinda Botswana Defence Forces (BDF) XI kwa mabao 2-0 jana kwenye Uwanja wa
Taifa, katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Wageni
walianza pambano la jana kwa kasi na walipoteza nafasi nzuri katika dakika ya
pili iliyopotezwa na mchezaji wake, Babeker Bakri, kabla ya Azam FC kuzinduka
katika dakika za nne na saba wakati Tchetche alipopoteza nafasi nzuri kwa
mashuti yake kudakwa na kipa Salim wa El Merreikh.
Baada ya bao
la Kavumbagu, El Merreikh walikosa bao katika dakika ya 21, baada ya Mkenya
Allan Wanga kupiga shuti kali baada ya kupokea pasi ya Abdallah Rage. Timu hizo
ziliendelea kushambuliana kwa zamu.
Dakika ya
35, Tchetche alishindwa kumtengenezea nafasi nzuri Kavumbagu afunge bao la pili
baada ya kipa wa El Merreikh kutoa pasi ya nyuma huku Mrundi huyo akiwa mbele.
Dakika mbili baadaye, Tchetche alipiga shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari
ambalo lilitoka nje ya goli.
Azam FC
ilikwenda mapumziko ikiwa mbele, na kipindi cha pili kilianza kwa El Merreikh
kufanya mabadiliko kwa kumtoa Kamal Amir na kuingia Mohamed Traore.
Dakika nne
baada ya kuanza kipindi hicho, Wanga alioneshwa kadi ya njano na mwamuzi Hassan
Mohammed wa Somalia kwa kushika mpira kwa makusudi, huku Aggrey Morris naye
akioneshwa kadi hiyo kwa kucheza rafu.
El Merreikh
walikianza kipindi cha pili kwa kasi na kupoteza nafasi mbili nzuri za mabao,
lakini Azam nao wakipoteza nafasi nzuri kupitia kwa nahodha Abubakar, kabla ya kumtoa Frank Domayo na kuingia
Himid Mao.
Dakika ya
62, kipa wa Azam FC, Aishi Manula aliokoa mpira wa tik-tak wa Traore, kabla ya
beki Erasto Nyoni kukaribia kuifungia timu ya Chamazi baada ya shuti lake
kugonga mlingoti wa juu wa lango na kutoka nje. Dakika mbili baadaye, Kavumbagu
alikosa bao akiwa amebaki na kipa wa El Merreikh.
Baada ya
hapo, na hasa baada ya kuingia Bocco, Azam FC inayofundishwa na Joseph Omog wa
Cameroon ilizidi kutakata kwa kulishambulia kwa nguvu lango la El Merreikh
kabla ya kumuingiza Amri Kiemba katika dakika ya 86 akichukua nafasi ya
Kavumbagu.

No comments:
Post a Comment