Mbunge wa
Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) ameshindwa kuwasilisha hoja
binafsi, kuitaka Serikali iwasilishe bungeni ripoti ya Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (Takukuru), kuhusu uchunguzi wa tuhuma za rushwa katika sakata la
iliyokuwa Akaunti ya Tegeta Escrow.
Lengo la hoja
hiyo kwa mujibu wa madai ya Kafulila, ilikuwa kuwezesha Bunge, kufanya uamuzi
mwingine wa alichoita ni uchunguzi mpana na wa kina.
Kwa mujibu wa
barua iliyotolewa na Bunge kwenda kwa mbunge huyo, ambayo gazeti hili limepata
nakala yake jana, Bunge limezuia hatua hiyo ya Kafulila, kwa sababu ilikuwa
inakiuka Kanuni za Bunge.
Utaratibu
uliowekwa na kanuni ya 54 (4) ya Kanuni za Bunge toleo la 2013, umekataza
hoja iliyokwishaamuliwa na Bunge, isijadiliwe ndani ya miezi 12 isipokuwa kama
ni hoja ya kutaka uamuzi huo wa Bunge uliokwishafanyika ubadilishwe.
Katika barua
hiyo iliyosainiwa na Pius Mboya, kwa niaba ya Katibu wa Bunge, imeeleza kwa
kuwa hoja ya Kafulila haikusudii kutaka uamuzi huo ubadilishwe, haikubaliki
kikanuni.
Barua hiyo
ilieleza kuwa suala hilo lilijadiliwa na kuhitimishwa na Bunge katika mkutano
wa 16 na 17 na kutolewa maazimio yanayotakiwa kutekelezwa na serikali, ikiwa ni
pamoja na Takukuru.
“Tunapenda
kukujulisha pia kwamba hakuna ibara yoyote ya Katiba wala kifungu chochote cha
Sheria, kinacholipa Bunge madaraka ya kuitaka Serikali iwasilishe bungeni
ripoti yoyote ya kiuchunguzi ya Takukuru, ili ijadiliwe bungeni,” ilieleza
sehemu ya barua hiyo.
Awali akizungumza
na waandishi wa habari mjini hapa, Kafulila alisema ripoti iliyojadiliwa awali
ilikuwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo inaangalia upungufu
wa kisheria, lakini Takukuru wanajadili mpaka kesi za jinai.
Alisema
kujadili ripoti ya Takukuru, kungewezesha kuweka wazi watuhumiwa kwa asilimia
70, wakati ile ya CAG ni asilimia 30 tu.
Kafulila
alisema baada ya kuzuiwa kutoa hoja yake binafsi, anajadiliana na wanasheria
wake kuangalia taratibu za kikanuni ndani ya mamlaka ya Bunge, ili kupata ushauri
nini cha kufanya.
Suala hilo la
utoaji wa fedha takribani Sh bilioni 200, kwa iliyokuwa akaunti ya Tegeta
Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT), baada ya kuamuliwa, Serikali, Bunge na
Mahakama vilipewa maazimio ya kutekeleza.
Tayari kwa
upande wa Serikali, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka aliondolewa katika nafasi yake, huku aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, wakijiuzulu.
Baada ya hapo,
Mahakama nayo imeshaanza utekelezaji kwa kuchunguza watendaji wake
wanaotuhumiwa, huku wenyeviti wa Bunge wawili, Andrew Chenge, aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na William Ngeleja, aliyekuwa Kamati ya Katiba,
Sheria na Utawala, wakijiuzulu nafasi zao bungeni.

No comments:
Post a Comment