Mtu anayetuhumiwa kwa utapeli, amekamatwa
wilayani Hanang’ mkoani Manyara akidaiwa kuwa na vyeti bandia vitatu vya ajira
tofauti akidai ni mwalimu, ofisa mifugo na polisi.
Mtuhumiwa huyo, Hamis Yusufu alikamatwa katika
kata ya Gissambalang’ wilayani Hanang kwa ushirikiano wa ofisi ya diwani pamoja
na polisi jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi,
Diwani wa kata ya Gissambalang’, Masala Bajuta, alisema mtu huyo
alikamatwa Januari 10 mwaka huu saa 11
kwenye shule ya sekondari Gissambalang’.
Alikamatwa
baada ya walimu kumtilia shaka akidai anafanya mazoezi kwa vitendo
shuleni hapo.
Kwa mujibu wa diwani, mtu huyo alifika shuleni
hapo na kupewa hifadhi na mmoja wa walimu baada ya kujitambulisha kwamba
amefika kufanya mazoezi kwa vitendo. Alipotakiwa kuonesha vitambulisho na vyeti vyake, alidai kuwa
alivisahau mjini Katesh.
“Huyu mtu Hamis Yusufu alikuwa haeleweki mara
aseme yeye ni mwalimu, mara yeye ni askari polisi wa upelelezi, mara yeye ni
ofisa mifugo na alipobanwa zaidi alidai kuwa yeye ni mwananchi wa kawaida tu,”
alisema Bajuta.
Alisema Polisi Jamii walipompekua walimkuta na
vyeti vitatu vilivyopigwa mihuri japokuwa vingine havikuwa na picha yake.
Alisema kitambulisho kimoja kilikuwa
na picha ya Ofisa Mifugo, George
Lwakatare ikionesha ameajiriwa mjini Singida.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara,
Christopher Fuime
alithibitisha kukamatwa kwa mtu huyo na kusema
anashikiliwa kwenye kituo cha Polisi Katesh wilayani Hanang’ kwa uchunguzi
zaidi.
“Tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na pindi
utakapokamilika tutamfikisha mtuhumiwa huyu mahakamani kwa kosa la kughushi
vyeti na kudanganya kuwa yeye ni mtumishi wa serikali ili hali siyo kweli,”
alisema Kamanda Fuime.

No comments:
Post a Comment