Watu wenye
ulemavu wa ngozi (albino) wanaoishi vijijini, wana hatari ya kupata magonjwa ya
saratani ya ngozi, kutokana na kutokuwa na elimu ya afya bora na utunzaji wa
ngozi.
Kauli hiyo
ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi mkoani Dodoma, Ludovick
Kowo, katika warsha ya mafunzo ya afya bora na utunzaji wa ngozi kwa albino
wilayani Kongwa.
Alisema kutokana
na ukosefu wa elimu ya utunzaji wa afya ya ngozi kwa walemavu waishio vijijini,
walemavu hao wana hatari kubwa ya kupatwa na saratani ya ngozi na kuongeza kuwa
ukosefu huo wa elimu, unatokana na umasikini.
Pia alisema
walemavu walio wengi, hawana elimu ya kutosha ya utunzaji wa afya zao, hali
inayochangiwa na ukosefu wa kipato cha kuwasaidia katika kujikwamua na hali
ngumu na ununuzi wa dawa hizo.
Akizungumza
kwenye mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la
Kufadhili Asasi za Kiraia (FCS), Kowo alisema Sh milioni 45 zimetolewa kwa ajili
ya utoaji wa elimu ya afya bora na utunzaji wa ngozi.
Alisema ufadhili
huo utaziwezesha wilaya mbili ikiwemo ya Kongwa na Mpwapwa na kata 12 kupata
elimu itakayowasaidia kuepukana na magonjwa hayo, ambayo yamekuwa tishio na
kusababisha vifo.
Mwenyekiti huyo
amezitaka taasisi na mashirika na serikali,
kuwezesha
walemavu kwa kuwapa mitaji, itakayowawezesha kuunda vikundi vya ujasiriamali
ili waondokane na hali ngumu ya maisha.
Alilitaka
shirika hilo kutoa kipaumbele katika utoaji wa elimu ya afya, kwa kuangaliza
zaidi walemavu wanaoishi vijijini, ambako wana changamoto nyingi za maisha
kuhusu namna ya kukabiliana na utunzaji bora wa afya zao.

No comments:
Post a Comment