MWAKYEMBE KUHAMISHWA WIZARA KWASHITUA WENGI
Mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri
yaliyofanywa Rais Kikwete mwishoni mwa wiki yamepokewa kwa hisia tofauti lakini
kubwa zaidi ni kuhamishwa kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kwenda
Wizara ya Afrika Mashariki, kumeonesha kugusa wengi, kutokana na wengi kuhoji
kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii.
Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bana alisema alitarajia Mwakyembe angeendelea
kubaki katika wizara hiyo ya uchukuzi, kutokana na mipango na mikakati mingi
aliyokuwa akiifanya katika kuendeleza sekta ya uchukuzi nchini.
“Katika hili, Rais angeangalia kwa jicho pana
zaidi kwa sababu tayari Mwakyembe alionesha kufanya vizuri katika kutatua
matatizo ya reli, kama vile Tazara na Bandari, ambayo hata hivyo pamoja na
jitihada zake bado yana matatizo,” alisema Dk Bana.
Hata hivyo, alipongeza hatua ya Rais kuamua
kumweka Samuel Sitta (aliyekuwa Wizara ya Afrika Mashariki) katika sekta hiyo
ya uchukuzi na kusisitiza kwamba
anaamini kutokana na uzoefu wa muda mrefu serikalini alionao, atafanya vizuri zaidi katika uchukuzi.
Dk Bana alisema kwa kuwa Mwakyembe ana uzoefu
mzuri katika masuala ya kimataifa, anatarajia kufanya vizuri katika wizara hiyo
ya Afrika Mashariki. Lakini, alidai ana wasiwasi juu ya utendaji wenye tija wa
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania (TPSF), Simbeye alisema anasikitishwa na kitendo cha Mwakyembe
kuhamishwa Wizara ya Uchukuzi kwa kile alichosema, tayari alikuwa anafanya
vizuri katika kusimamia maboresho ya reli na bandari.
“Lakini napenda kusisitiza kuwa Sekta binafsi
tunaahidi kutoa ushirikiano kwa mawazri wote wapya,” alisema.
Simbeye alisema taasisi hiyo imepokea kwa
furaha uteuzi wa George Simbachawene kuwa Waziri wa Nishati na Madini, kwa kuwa ana uzoefu mkubwa katika masuala ya
nishati na madini.
Aidha alisema taasisi hiyo inatarajia waziri
huyo atasimamia kupitia Baraza la Mawaziri, kupitishwa kwa Sera ya gesi yenye
kipengele cha nafasi ya wazawa kuweza kushiriki katika miradi ya gesi na mafuta
nchini.
Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Rais Kikwete aliteua naibu mawaziri
wawili wapya na kupandisha cheo wawili huku mawaziri wengine sita
walibadilishwa nafasi zao, hatua iliyochukuliwa pia kwa naibu mawaziri watatu.
Sura mpya mbili, yupo Mbunge wa Same
Mashariki, Anne Kilango Malecela, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, kuchukua nafasi ya Jenista Mhagama.
Mwingine ni Mbunge wa Muleba Kaskazini, John
Mwijage, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, kuchukua
nafasi ya Steven Maselle.
Naibu Waziri waliopandishwa cheo ni pamoja na
Mhagama, ambaye sasa anakuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na William Lukuvi.
Mwingine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene, ambaye ameteuliwa kuwa
Waziri wa Nishati na Madini, nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Muhongo.
Kati ya waliobadilishwa nafasi zao ni
aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye sasa
ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi, nafasi aliyokuwa nayo Dk Harrison
Mwakyembe.
Mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu, ambaye sasa anakuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Mahusiano na Uratibu, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Stephen Wassira.
Christopher Chiza, aliyekuwa Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Uwekezaji na Uwezeshaji, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Dk Nagu.
Dk Mwakyembe ameteuliwa kushika nafasi ya
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, iliyokuwa ikishikiliwa na Sitta,
huku Wassira akiteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika nafasi
iliyokuwa ikishikiliwa na Chiza.
Aidha, Lukuvi ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Tibaijuka,
ambaye aliondolewa katika wadhifa huo kutokana na kashfa hiyo.
Katika safu na naibu mawaziri waliobadilishwa
vyeo, yupo aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Maselle ambaye sasa
amekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano.
Mwingine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba
na Sheria, Angela Kairuki, ambaye anakuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, nafasi iliyoachwa wazi na
Simbachawene.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais Mazingira, Ummy Mwalimu, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa BoT
mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji
(capacity charges) zilizokuwa zinalipwa na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa
anayelipwa, ambaye ni kampuni binafsi ya
kufua umeme ya IPTL. Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa
IPTL, lakini baadaye Tanesco ililalamikia
kiwango chake. Kimsingi, fedha
zilizokuwa katika akaunti hiyo ni za IPTL, kwani ndiye mlipwaji na ni
malipo yanatokana na madai ya IPTL kwa TANESCO kuhusu tozo ya uwekezaji.
Katika mabadiliko hayo madogo sanjari na
kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kumeelezwa kuwa kumenusuru Bunge na msuguano
usio na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Watu wa kada tofauti waliozungumza jana,
walisema mabadiliko hayo na kuondoka kwa Muhongo, kumesaidia kufilisi hoja za baadhi ya
wabunge, ambao wangeendelea kutumia sakata la ufisadi katika akaunti ya Tegeta
Escrow ya iliyokuwa Benki Kuu (BoT), kujijenga binafsi kisiasa.
Wasomi walisema hatua hiyo itaondoa msuguano
wa muda mrefu, ulikuwapo ndani ya Bunge na hata kwenye jamii kwa ujumla.
Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili ni
Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ayoub Rioba, aliyesema mabadiliko hayo
yataondoa msuguano miongoni mwa wabunge, kwani wangeweza kukasirishwa kama
kusingekuwa na mabadiliko.
Rioba alisema mabadiliko hayo madogo, ilikuwa
lazima yatokee, kutokana na Serikali kuwa na wajibu wa kutekeleza mapendekezo
ya Bunge juu ya sakata hilo la akaunti ya Escrow.
Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema kutokana na hatua hiyo ya
kuwaondoa baadhi ya mawaziri waliohusishwa na sakata hilo, Rais Kikwete
ametumia fursa nzuri katika utekelezaji wa maazimio ya Bunge.
Katika maazimio manane ya Bunge, mojawapo
lilikuwa ni kuwawajibisha Waziri wa
Nishati na Madini, Muhongo, Katibu Mkuu
wa wizara hiyo, Eliakim Maswi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema Watanzania wengi waliyategemea
mabadiliko hayo, kutokana na sakata hilo
lilivyotikisa Bunge.
Baadhi ya watu waliopiga simu kwenye chumba
cha habari, ingawa walikosoa hatua ya Muhongo kuchelewa kujiuzulu, walisema
kuondoka kwake kutafanya mkutano huo wa Bunge unaoanza kesho, kujadili mambo
muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja.
“Napongeza hatua zilizochukuliwa, ingawa
Muhongo alichelewa kujiuzulu, lakini sasa kuondoka kwake tunaamini tutapumua na
suala hili la Escrow. Hata bungeni sasa wabunge wetu watajadili mambo muhimu
yanayotugusa moja kwa moja badala ya wanasiasa kuchuana wenyewe kwa wenyewe
kutafuta umaarufu,” alisema mkazi wa
Mwanza, Joseph Kalisa.
Kile kilichoonekana kwamba suala la Escrow
lingeendelea kuwasha moto katika mkutano wa Bunge unaoanza kesho, ni kauli
zilizokuwa zimeanza kutolewa hivi karibuni na baadhi ya wabunge wa upinzani.
Kauli hizo zilionesha kwamba suala hilo
lingeendelea kuwa mtaji wao wa kisiasa.
Miongoni mwa wabunge hao ni Mbunge wa Arusha
Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyedai angemtoa kwa mabavu bungeni Muhongo
katika kikao kijacho cha Bunge, endapo angekuwa hajaondolewa kwenye nafasi
hiyo.
Mkakati huo wa Lema uliungwa mkono na Mbunge
wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ambaye pia alikaririwa akisema
amepanga kumtoa bungeni kwa nguvu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti,
Andrew Chenge anayehusishwa pia na sakata hilo.
Akizungumzia ya Muhongo kujiuzulu, Dk Rioba
alisema ni hatua ya kiungwana ingawa alichelewa kuchukua uamuzi huo, hivyo
kuruhusu mashambulizi dhidi yake yasiyo na sababu.
“Muhongo ni msomi na kwa hadhi yake ametoa
mchango mkubwa kwa nchi kabla ya kuwa waziri na wakati akiwa waziri. Lakini
tangu suala hili litokee alitakiwa kuchukua uamuzi huu mapema, kwani kuchelewa
kwake kumekaribisha ‘mawe’ bila sababu na angewahi ingesaidia sana,” alisema Rioba.
Wakati watu mbalimbali wakiamini kwamba
kujiuzulu kwake kutaleta tija kwenye Bunge linaloanza kesho, pia kwa upande
wake, Muhongo, miongoni mwa sababu alizotoa wakati akijiuzulu
ni kwamba yeye ni suluhisho la mjadala wa sakata hilo la Escrow.
Alisema aliona achukue uamuzi huo, serikali ipate nafasi ya kushughulika na
matatizo ya Watanzania, badala ya kutumia muda mrefu katika mjadala huo.
Alisema uamuzi wake, utatoa nafasi kwa CCM
kuendelea kutafuta suluhisho la kero za Watanzania, badala ya kutumia vikao
kujadili suala hilo.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Madini ya Stamigold, Denis Sebugwao, alimshukuru
Muhongo kwa kuunga mkono na kuwezesha uundaji wa kampuni hiyo ya kwanza ya
serikali ya kumiliki madini.
Hata hivyo, alisema wanawakaribisha mawaziri wapya,
akiamini watamsaidia Rais kukidhi matarajio yake ya kuhudumia umma.
Comments