MIJADALA YA WIZI, UFISADI SASA YAWACHOSHA WABUNGE
Wabunge
wameelezea kuchoshwa na wizi, matumizi mabaya ya fedha na mikataba mibovu
iliyobainishwa katika taarifa za baadhi ya kamati zilizowasilishwa bungeni, na kushauri maazimio yapitishwe ili wahusika wa ufisadi huo wabanwe.
Katika
kuchangia taarifa za Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya
Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Kamati ya Bajeti zilizowasilishwa bungeni,
wabunge wengi wameeleza kuchoshwa na mijadala ya kila mara bungeni
inayohusu wizi na ufisadi, badala ya kujadili maendeleo ya wananchi.
Kwa
mujibu wa wabunge hao, katika taarifa zote zilizowasilishwa, suala
la wizi na matumizi mabaya ya fedha za Serikali limejitokeza kwa wingi,
jambo ambalo wabunge wametaka hatua za makusudi zichukuliwe haraka, kuliko
wabunge kuendelea kulalamika bila kupata suluhu la kudumu.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF) alitoa mfano wa suala Kampuni ya Ndege (ATCL) lililoainishwa kwenye taarifa ya PAC juu ya hali ya kifedha na madeni makubwa iliyo nayo.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF) alitoa mfano wa suala Kampuni ya Ndege (ATCL) lililoainishwa kwenye taarifa ya PAC juu ya hali ya kifedha na madeni makubwa iliyo nayo.
Madeni
hayo ni pamoja mabilioni ya fedha yanayoendelea kulipwa kwa Kampuni ya Wallis,
kwa huduma ya ndege iliyofanya kazi nchini kwa miezi sita pekee, na kisha ndege
kupelekwa Ufaransa kwa matengenezo.
Alisema
chanzo cha tatizo ni mikataba mibovu. “Tulidai mikataba iletwe bungeni
tuipitie. Ikiwa tutaendelea kulalama kwamba tunaibiwa… wizi kila mahali, ikiwa
hatutasaidia Takukuru (Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa) kama Bunge kwa
kuona kwamba wote waliohusika na mikataba wanafikishwa mahakamani, itakuwa
Bunge hatujatenda haki.
“Kwa
kamati ambazo zimewasilisha taarifa, tupitishe maazimio kwa mikataba yote yenye
utata na walioipitisha, wafikishwe mahakamani. Tulione Bunge likiwa na meno
yake, wote waliohusika wachukuliwe hatua kwa kupelekwa mahakamani,“ alisema.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), alizungumzia suala la Mamlaka ya Bandari
(TPA) kutumia Sh bilioni tisa kulipana posho bila kuidhinishwa na Ofisi ya
Msajili wa Hazina; taarifa iliyotolewa na PAC.
Bulaya
alihoji majibu ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, ambaye juzi katika kujibu,
alisema TPA walijieleza kwamba walifanya hivyo kutokana na kutokuwa na uelewa
wa sheria. “Eti jibu jepesi, hawakuwa na uelewa wa kisheria!. Tunaomba
watu wote hao washughulikiwe. Haiwezekani makosa yawe yale yale na majibu yale
yale,” alisema Bulaya.
Kuhusu
madeni ambayo mifuko ya hifadhi ya jamii inadai Serikali, Bulaya alisema; “Kila
siku zinapigwa kelele juu ya hali mbaya ya mifuko ya jamii, halafu Waziri
anasema kinaundwa kikosi kazi…hiki ni kikosi kazi cha kumi, hivyo tisa
havijajua tunadaiwa kiasi gani?”
Kwa
upande wa jengo la watu mashuhuri katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere, mbunge huyo alihoji uhalali wa kutumika Sh bilioni 12 kwa
ujenzi wake.
“Dili
nyingine ukipewa funga mikono, nawa mikono zinagusa maisha ya watu maskini,”
alisema.
Bulaya
ambaye pia alihoji sababu za asilimia 10 ya fedha za akina mama na vijana
kutotengwa kwenye halmashauri, alishauri mawaziri kubana watendaji iwapo
hawataki kupigiwa kelele bungeni.
Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema iwapo wizi hautadhibitiwa,
nchi haiwezi kubadilika hata ikikusanya matrilioni ya shilingi.
“Ni
lini tutajadiliana bungeni bila kujadili wizi? Ifike hatua tujadili sera za
kuendeleza Taifa,” alisema Mbunge huyo na kuongeza kuwa CUF na Chadema haviko
kwa ajili ya kushika madaraka tu, bali ni kwa ajili ya kuwezesha taifa kwenda
mbele. Aliongeza kuwa kama CCM ikiongoza vyema kukawa na maendeleo, itakuwa
sawa.
Alisema
katika taarifa ya PAC mwanzo hadi mwisho, kinachosomwa zaidi ni wizi, jambo
alilotaka Serikali kushughulikia watu wanaojenga nyumba kwa mikataba ya uongo
sanjari na ulipaji mishahara hewa.
Pia Mbunge
wa Nkenge, Asumpta Mshama (CCM) alihoji ni lini bunge litaelezwa kwamba
matumizi ya fedha sasa yanakwenda vizuri.
Mshama
alishauri sheria ya ununuzi iletwe bungeni waibadilishe kwa kile alichosema,
inatoa mwanya mkubwa wa kufanya matumizi mabaya ya fedha.
Comments