Polisi wa kituo
cha Kinesi wilayani Rorya mkoani Mara, Konstebo Deogratius amejeruhiwa kwa
kuchomwa mkuki ubavuni.
Alichomwa mkuki
wakati akiwa na wenzake walipokuwa wakipambana kujaribu kuwaondoa zaidi ya watu
2,000 waliovamia mgodi wa dhahabu wa kampuni ya Acacia wa North Mara uliopo
Nyamongo wilayani Tarime.
Askari huyo
mwenye namba G 7606 amelazwa katika Hospitali ya Shirati akitibiwa jeraha hilo.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa alisema kuwa kutokana
na uvamizi huo, polisi inawashikilia watu sita wanaotuhumiwa kuingia ndani ya
mgodi na kujeruhi baadhi ya askari akiwamo huyo aliyechomwa mkuki kwa lengo la
kuiba mawe ya dhahabu.
Kamanda huyo
alibainisha kuwa watu hao zaidi ya 2,000 waliingia ndani ya mgodi huo, saa 7:00
mchana wakiwa na silaha za jadi kama vile mapanga, mishale, mikuki na marungu.
“Waliingia
ndani ya mgodi na kuanza kufanya vurugu kwa kuwashambulia askari na walinzi
waliokuwa wakilinda mgodi huo kwa nia ya kutaka kupora mawe ya dhahabu,”
alisema na kuongeza:
“Askari wetu wa
Jeshi la Polisi wakishirikiana na walinzi wa mgodi huo waliwazuia wavamizi hao
kwa kurusha mabomu ili wasiingie kupora mali.
“Walijitahidi kupambana na kundi hilo la
wavamizi hao na kufanikiwa kuwaondoa ndani ya mgodi huo, lakini askari wetu PC
Deogratius aliyekuwa katika operesheni hiyo alijeruhiwa na mkuki ubavuni”.
Alisema
alikimbizwa kupatiwa matibabu ya awali katika Hospitali ya Wilaya Tarime na kwa
sasa amehamishiwa kupata vipimo vya x-ray katika Hospitali ya Shirati wilayani
Rorya ambapo anaendelea na matibabu.
Alisema watu sita wanaoshikiliwa na polisi
wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma za kuvamia na
kuingia ndani ya mgodi bila idhini wakiwa na lengo la kufanya uhalifu na
kujeruhi askari.

No comments:
Post a Comment