Tuesday, December 30, 2014

AJALI YAUA WANNE MOSHI, YAJERUHI WATATU HANDENI

Watu wanne wamekufa na watatu wamejeruhiwa katika ajali mbili tofauti, zilizotokea Moshi mkoani Kilimanjaro na Handeni mkoani Tanga.

HAKIMU AJITOA KESI YA UGAIDI YA SHEKE FARID

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Riwa amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake. 

MAMLAKA HALI YA HEWA YASEMA MSIMU WA MVUA UMEKWISHA

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema msimu wa mvua za mwisho wa mwaka unaisha leo, ingawaje bado inatarajiwa kuwa na mvua kuanzia mapema mwaka 2015.  

MWANAFUNZI AJIZOLEA MILIONI 3/- ZA BIMA KUTOKA BAYPORT

Taasisi ya kifedha inayojihusisha na utoaji wa mikopo ya Bayport Tanzania, imempatia Sh milioni tatu mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu kishiriki cha Mkwawa (MUCE), Kennedy Kaupenda, kufuatia huduma mpya ya Bima ya Elimu inayoendeshwa na taasisi hiyo nchini.

Monday, December 29, 2014

MVUA KUBWA DAR MAJANGA, MTOTO ASOMBWA AKIWA AMELALA


Hivi ndivyo hali ilivyokuwa jijini Dar es Salaam baada ya mvua kubwa kunyesha kwa takribani saa mbili mfululizo.
Mvua iliyonyesha jijini Dar es Salaam, imeleta balaa baada ya kuua watu wawili, katika maeneo tofauti ya jiji, likiwemo tukio la mtoto wa miaka minane kufa baada ya kuzidiwa na maji yaliyoingia ndani ya nyumba aliyokuwa amelala.

'WALIOMUUA' DK SENGONDO MVUNGI WALETA KIZAZAAZAA KORTINI


Washitakiwa wa kesi ya mauaji ya Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Edmund Mvungi (pichani), jana waligoma kutoka katika chumba cha mahakama na kukaa kizimbani kwa muda hadi watakapoelezwa jalada la kesi yao lipo wapi.

AJIZALISHA NA KUTUMBUKIZA KICHANGA KWENYE NDOO


Msichana mmoja mkazi wa Mtaa wa Zaire eneo la Kijenge Kaskazini mkoani Arusha, amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru chini ya ulinzi mkali wa Polisi baada ya kujizalisha mwenyewe na kisha kumtumbukiza mtoto wake kwenye ndoo ya maji.

BENKI YA MKOMBOZI YATINGA KWA KISHINDO SOKO LA HISA DAR


Hisa za benki ya biashara ya Mkombozi,  jana ziliingia kwenye  Soko la  Hisa la Dar es Salaam  (DSE) kwa kishindo huku bei yake ikipanda kwa asilimia 50 kutoka Sh 1,000 hadi 1,500.

WATU 21 WANUSURIKA KIFO AJALINI WAKITOKA HARUSINI


Mtu mmoja amekufa na wengine 21 kujeruhiwa, baada ya basi dogo aina ya Coaster walilokuwa wakisafiria kutoka Shinyanga kwenye harusi, kurejea nyumbani kwao Morogoro kupinduka katika kijiji cha Ikugha wilayani Ikungi kwenye barabara kuu ya Singida - Dodoma.

DEREVA WA BODABODA AUAWA NA KUTUNDIKWA KWENYE MTI


Mwendesha pikipiki (bodaboda), mkazi wa Kitongoji cha Buriba katika mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, Mrimi Nyabikwi (23), amekutwa amekufa na mwili wake kukutwa umening'inizwa kwenye mti maeneo ya Makaburini.
Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa amethibitisha kifo hicho. Alisema habari kutoka ndani ya familia ya  mtu huyo zilidai kuwa Mrimi alitoweka nyumbani kwake kuanzia Desemba 24, mwaka huu.
Alisema marehemu alikuwa amekodisha pikipiki ya mkazi wa Sirari kwa kufanyia kazi ya kusomba abiria, lakini hakurejea nyumbani hadi mwili wake ulipokutwa na wachungaji wa mifugo maeneo ya makaburi katika mji huo wa Sirari. Mwili wa mtu huyo ulikuwa umeanza kuharibika.
Alisema kuwa mwili wa mtu huyo, ulifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Wilaya na kisha kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa maziko.

YASEMAVYO MAGAZETI YA JUMANNE - DESEMBA 30

Friday, December 26, 2014

POLISI ACHOMWA MKUKI UBAVUNI MKOANI MARA


Polisi wa kituo cha Kinesi wilayani Rorya mkoani Mara, Konstebo Deogratius amejeruhiwa kwa kuchomwa mkuki ubavuni.

BUBU AFANYIWA UNYAMA, ABAKWA NA WATU WATANO

Mkazi  wa kitongoji cha Chingale, kijiji cha Mtakuja kata ya Temeke katika Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara ambaye ni bubu, Asumini Fakihi amebakwa na watu watano wasiojulikana na kumsababishia majeraha na kulazwa katika Hospitali ya Mkomaindo mjini Masasi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Agustino Ollomi alisema juzi saa 1:00 usiku wa mkesha wa Krismasi katika kitongoji  cha Chingale, mama huyo alivamiwa na watu hao wasiofahamika waliofanikiwa kumfanyia kitendo hicho na kutokomea kusikojulikana.

VITONGOJI 11 HAVIKUPIGA KURA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA


Wakazi wa vitongoji 11 katika  vijiji vitatu vya  halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wameshindwa kupiga kura kuchagua viongozi wa serikali za vitongoji na vijiji, kutokana nna migogoro ya ardhi iliyopo kwenye vitongoji hivyo.

ALIYELAWITI MTOTO WA MIAKA SITA ATUPWA JELA

Mfanyakazi wa nyumbani, Hatibu Adamu (20) amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kike wa miaka sita.

KRISMASI YASHEREHEKEWA KWA AMANI DAR

Hali ya usalama katika jiji la Dar es Salaam imeelezwa kuwa shwari katika sikukuu ya Krismasi huku ulinzi ukiimarishwa zaidi kuelekea mwisho wa mwaka.
Jiji hilo lenye mikoa mitatu ya Kipolisi ya Ilala, Kinondoni na Temeke, hakuna matukio makubwa yaliyojitokeza.

HOTUBA KAMILI YA RAIS KIKWETE ALIPOZUNGUMZA NA WAZEE WA DAR ES SALAAM


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA MKOA WA DAR ES SALAAM,
TAREHE 22 DESEMBA, 2014
Shukrani
Mheshimiwa Makamu wa Rais;
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi wa CCM Mkoa;
Viongozi Wenzangu;
Viongozi wa Dini;
Wazee Wangu;
Wananchi Wenzangu; 
Nawashukuru sana wazee wangu wa Dar es Salaam, kwa kukubali mwaliko wangu na kuja kuzungumza nami siku ya leo.  Natambua kuwa taarifa ilikuwa ya muda mfupi, lakini mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki.  Naomba radhi kwamba ilikuwa tukutane Ijumaa lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu, tukaahirisha mpaka leo. Asanteni sana kwa uvumilivu wenu.  
Kama mjuavyo, kila ninapoomba kukutana nanyi ninalo jambo au mambo muhimu kitaifa, ambayo napenda kuzungumza nanyi, na kwa kupitia kwenu, taifa zima linapata habari.  Leo nina mambo mawili:
Wazee Wangu;
Kwanza kabisa, nataka kurudia kuwashukuru Watanzania wenzangu kwa moyo wenu wa upendo, mliouonyesha kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu nikiwa nje na hata baada ya kurejea nchini. Kwa kweli nina deni kubwa kwenu.    Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba watu wamekuwa wananiombea uponyaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa na kunitia moyo.  Nadhani zimechangia sana kuifanya afya yangu, kuendelea kuimarika kila kukicha.  Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo ilivyokuwa wiki iliyopita au siku niliporejea nchini.

Thursday, December 25, 2014

WANANDOA WAUAWA KWA KUCHARANGWA MAPANGA MKOANI MARA...

Watu wawili ambao ni wanandoa wameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana na kisha wauaji hao kuchukua baadhi ya viungo vyao katika kitongoji cha Mwabasabi, wilaya ya Bunda, mkoani Mara.

LOWASSA APONGEZA AMANI KISIWANI ZANZIBAR

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewapongeza Wazanzibar na Serikali ya mseto visiwani humo kwa kudumisha amani.
Akitoa salamu zake Krismasi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  Mwanakwerekwe mjini Unguja alikokwenda kusali, Lowassa (pichani) ambaye ni Mbunge wa Monduli mkoani Arusha, alisema hali ya amani visiwani humo sasa ni shwari kabisa.

WATOTO 53 WAONDOKA LEO KWENDA INDIA KWA MATIBABU

Watoto 53 wanaougua maradhi mbalimbali ya moyo wanaondoka nchini leo kwenda India kwa upasuaji ambapo wataagwa na Makamu wa Rais, Dk Ghalib Bilal.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mratibu wa magonjwa ya moyo katika Klabu ya Lions ya Dar es Salaam jana, Dk Rajni Kanabar (pichani), wagonjwa hao watatibiwa katika hospitali mbalimbali nchini India.

TBS YAFUNGIA KIWANDA CHA KUZALISHA JUISI ZA U-FRESH

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekifunga kwa muda usiojulikana kiwanda cha U-Fresh Food Limited cha Tegeta Dar es Salaam, kwa kuzalisha juisi ya U-Fresh chini ya kwa kiwango cha ubora unaotakiwa.

Friday, December 5, 2014

MDAU WA BLOGU YA ZIRO99 AAMUA KUCHANA NA UKAPERA...

Ilikuwa furaha, nderemo na vifijo!! Wakiwa na nyuso za furaha Bwana Elijah Eusebio Kitosi na Bi Upendo Deogratius Lufundya mara baada ya kufunga pingu za maisha kwenye Kanisa Katoliki la Maximillian Kolbe, Mwenge, Dar es Salaam Novemba 29, mwaka huu. Bwana harusi ni mwajiriwa wa kampuni ya Primefuels Ltd na Bi Harusi ni mwajiriwa wa Benki ya Posta.
Wakiwa wenye furaha, maharusi Elijah na Upendo pamoja na wapambe wao mara baada ya kufunga ndoa takatifu kwenye Kanisa Katoliki la Maximillian Kolbe-Mwenge, Dar es Salaam Novemba 29, mwaka huu. Watoto waliosimama mbele ni Thobias Mbagga na Celine Aggrey Kitosi.
Mdau wa blogu hii, Elijah Eusebio Kitosi akiwa mwenye furaha baada ya kukabidhiwa mke, Upendo Deogratius Lufundya wakati wa sherehe ya Send-Off iliyofanyika jijini Arusha Ijumaa ya Novemba 21, mwaka huu kwenye Ukumbi wa City Link.
Mzee Eusebio Kitosi, baba mzazi wa Elijah akitabasamu wakati wa sherehe ya Send-Off kwenye Ukumbi wa City Link, jijini Arusha Novemba 21, mwaka huu. Kulia ni mshenga, Bw David Koya.
Dada zake Elijah Eusebio Kitosi wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa sherehe ya Send-Off iliyofanyika Ijumaa ya Novemba 21, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Hoteli ya City Link, maeneo ya Phillips, jijini Arusha. Kutoka kulia ni Zitta Mgonja na Regia Fivawo. Kushoto ni Agnes Fivawo, mpwa wa Elijah.