SERIKALI YAOKOA SHILINGI BILIONI 40 ZA MISHAHARA HEWA


Serikali imeokoa Sh bilioni 40  zinazodaiwa zilikuwa zikiingia kwenye mifuko ya watu wachache kutokana na ulipaji wa mishahara hewa.
Naibu  Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alitoa kauli hiyo  kwenye mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi hivi karibuni wilayani Igunga katika Mkoa wa Tabora.
Alisema fedha hizo zilikuwa zikipotea kila mwezi na baada ya kufanya uhakiki, iligunduliwa kulikuwepo watumishi hewa 14,000 miongoni mwao wakiwa marehemu, waliokuwa wakilipwa mshahara kila mwezi.
Alisema baada ya kugundua,  serikali iliamua kulipa mishahara ya watumishi kwa kuweka kwenye akaunti zao moja kwa moja na ndipo ilipobaini wizi huo.
Mwigulu alisema serikali imepeleka suala la udanganyifu na wizi huo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)  na wahusika wote watakaogundulika watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Alisema wahusika wameibia taifa kwa muda mrefu hivyo wajiandae kisaikolojia kwani safari hii serikali imeamua kuingiza taifa kwenye kipato cha kati.
Akielezea namna wizi unavyofanyika, Mwigulu alitoa mfano wa Sh bilioni 48 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ununuzi wa dawa lakini baada ya ukaguzi, iligundulika Sh bilioni saba ndizo zilinunua dawa na Sh bilioni 41 ziliibwa.
Alisema wakati serikali ikifanya uhakiki kwenye huduma za wazabuni na kuamua kulipa deni la ndani la taifa imegundulika Sh  bilioni 500 zilikuwa kama deni lakini deni sahihi baada ya uhakiki ni Sh bilioni 140.
Alisisitiza serikali  itafukuza wahusika wote na kuajiri wapya katika kudhibiti  wizi serikalini.
Kwa mujibu wa Mwigulu, serikali itaendelea kufuatilia kila fedha zinapotolewa. Kwa mujibu wake, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2014/2015, imeshatoa Sh bilioni 250 kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini.

No comments: