TANZANIA KUONGOZA KWA WATAALAMU WA GESI AFRIKA

Utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, ya kumwachia mrithi wake mazingira ya kuongoza nchi tajiri, umeanza kutoa mwanga, ambapo Tanzania sasa inajiandaa kuongoza Afrika kwa kuwa na wataalamu wazawa wa mafuta na gesi.
Jana Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitangaza kuwa katika miaka mitano ijayo, Tanzania itakuwa na wataalamu zaidi ya 300, watakaokuwa wamebobea katika masuala hayo kutoka katika vyuo mbalimbali vya kimataifa.
Aidha, wakati Serikali ikitarajia kuwa na wataalamu hao miaka mitano ijayo, yaani 2020, ni wakati huo huo Tanzania itakuwa ikianza kupokea mapato yake ya kwanza kutokana na rasilimali hiyo.
Idadi hiyo ya wataalamu kwa mujibu wa Profesa Muhongo, itasababisha Tanzania kuongoza Afrika kwa kuwa na wataalamu wa rasilimali hiyo wazawa na kufanya sekta hiyo muhimu kwa mkakati wa kufuta umasikini kwa Watanzania, kushikiliwa na wazawa.
Mbali na kufikia hatua hiyo, matarajio hayo yanayotokana na hatua zilizoanza kuchukuliwa sasa, yatakuwa yametimiza maono ya Rais Kikwete ya kumwachia mrithi wake misingi ya Tanzania tajiri.
“Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Watanzania na nchi yao, wananufaika na mapato ya raslimali kutokana na gesi asilia. Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini.
“Rasilimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri.
“Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa kati ya sasa na mwisho wa kipindi changu cha uongozi, ni kuongoza nchi yetu kwenda kwenye njia hiyo, ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora zaidi kwa wananchi wetu,” alisema Rais Kikwete wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na Watanzania wanaoishi Marekani.
Katika kufanikisha maono hayo, Profesa Muhongo alisema Rais Kikwete na yeye, waliwaomba wataalamu wazawa zaidi ya 10 waliokuwa wakifanya kazi nje ya nchi, hasa Uingereza na Canada, warejee nyumbani kuja kusaidia kujenga nchi yao na wamekubali.
Mbali na kufanikiwa kurejesha wataalamu hao kutoka nje ya nchi, Profesa Muhongo alisema Serikali imeongeza kasi ya kupeleka wasomi nje ya nchi, kusoma masuala hayo katika ngazi mbalimbali ikiwemo za shahada za uzamili na shahada za uzamivu.
Katika muendelezo wa kasi hiyo, jana Profesa Muhongo alikabidhi hati za kuishi China (visa) kwa wanafunzi 10 wa kitanzania,  wanaoenda kusomea mafuta na gesi kwa ufadhili wa nchi hiyo, ambapo wanafunzi tisa watasomea shahada ya uzamili na mmoja shahada ya uzamivu (PhD). 
Alifafanua kwamba ufadhili wa masomo hayo kwa nchi ya China ulianza mwaka jana walipopeleka wanafunzi 10, na mwaka huu wamepeleka wengine 10 baada ya kuona maendeleo mazuri ya wale wa awali.
Kutokana na mafanikio hayo, Profesa Muhongo alisema  mwakani Serikali itapeleka wanafunzi wengine 20 nchini China.
Mbali na China, Profesa Muhongo alisema pia  kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, Norway itafadhili wanafunzi 40 katika fani hiyo katika ngazi ya shahada ya uzamivu (PhD), ambao watarejea nchini kuja kufundisha katika vyuo mbalimbali nchini.
Alisema pia kuna wanafunzi 15 wanaoendelea na mafunzo ya lugha ya Kireno katika ubalozi wa Brazil nchini, ili mwakani waende nchini humo  kusomea utaalamu huo wa mafuta na gesi.
Profesa Muhongo alisema Brazil, imejitolea kufadhili wanafunzi 10, lakini Wizara ya Nishati na Madini, itajitahidi ili wote 15 wapate fursa ya kwenda kusomea utaalamu huo.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, nchini Uingereza wapo wanafunzi zaidi ya 10. Mwakani watapeleka wanafunzi wengine katika nchi za Canada na Uingereza, kusoma shahada za uzamili na uzamivu, wakiwemo waandishi wa habari ili wapatikane waliobobea katika sekta hiyo na kusaidia kuelimisha jamii.
“Napenda kuwaalika waandishi wa habari kujitokeza kuleta maombi na wengine pia wenye uwezo wa kusomea sekta hiyo, waje kupata nafasi za masomo ya muda mrefu kwani mafunzo ya muda mfupi hayana tija,“ alisema Profesa Muhongo.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakimu Maswi  alitaja wanafunzi waliopewa hati za kuishi China jana  kuwa ni  Erasma Rutachura, ambaye ni mwanamke wa kwanza nchini kusomea masomo hayo katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD).
Wengine wanaosoma katika ngazi za Shahada ya Uzamili ni Abel Masanja, Beatrice Tubuke, Faustine Matiku, Alvin Mulashani, Kanugula Lwakutubi, Nigel Kimaro, Ansila Kiusa, Herbert Msangi na Victor Mugarula.
“Nafasi hizi zimepatikana kwa ushindani baada ya kutangazwa kwenye vyombo vya habari, ambapo vigezo vilivyotumika kupata ufadhili ni aina ya kozi aliyosoma mwombaji katika shahada ya kwanza au
uzamili, chuo alichosoma, kiwango cha ufaulu, GPA 3.0 na uwiano wa kijinsia,“ alisema Maswi.
Maswi alitoa mwito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hizo za ufadhili wa masomo mara zinapotolewa, ili watumie elimu hiyo kwa maendeleo endelevu ya sekta za nishati na madini.

No comments: