Tuesday, July 15, 2014

WAMA YATAFUTA 'DAWA' KWA MILA KANDAMIZI

Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Segal Family Foundation imeingia mkataba wa kufanya kazi na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) kuhakikisha jamii iliyosahaulika, inapata huduma muhimu.
Wama inaongozwa na mke wa Rais, Salma Kikwete. Taasisi ya Segal Family Foundation yenye makao makuu nchini Marekani, imewekeza katika nchi mbalimbali za Afrika
kwa kuzisaidia taasisi zisizo za kiserikali katika nchi hizo kuzisaidia jamii katika kufikia maendeleo.
Mama Salma alisema juzi kuwa taasisi hiyo imelenga zaidi kuwasaidia hasa watoto wa kike katika nchi mbalimbali barani Afrika kujiepusha na mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya  virusi vya Ukimwi tatizo ambalo bado ni kubwa katika nchi hizo.
Aliongeza kuwa mkataba huo utawezesha kuwafikia wasichana walio na umri kati ya miaka 14 hadi 24 kujiepusha na ndoa za utotoni kwa kutoa elimu.
Kwa mujibu wa Mama Salma, jamii lengwa ni zenye mila, desturi na tamaduni zinazomkandamiza mtoto wa kike na kuhakikisha zinabadilika na kumwona mtoto wa kike kuwa ana haki sawa na mtoto wa kiume.
Mkutano huo uliofanyika jijini Arusha  kwa siku tatu na ulishirikisha viongozi mbalimbali wa nchi za Kiafrika, mashirika mbalimbali na tassisi zisizokuwa za Kiserikali za Kimataifa. Walishirikisha uzoefu wa jinsi tatizo hilo lilivyo na jinsi ya kukabiliana nalo.

No comments: