WAKUU WA MIKOA WAPASHWA MIGONGANO NA MAKATIBU TAWALA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala nchini, kuheshimiana.
Pia, amewataka watambue kuwa wote ni wateule wa Rais, hivyo wanatakiwa wawe na uhusiano na mawasiliano mazuri ili kuwatumikia kwa ufanisi wananchi.
Balozi Iddi alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa.
Mafunzo hayo yameandaliwa na kufadhiliwa na Taasisi ya Uongozi.
 Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, alisema kumekuwa na changamoto ya uhusiano na muingiliano wa kiutendaji miongoni mwa wakuu hao wa mikoa na makatibu tawala.
Alisema  hali hiyo imesababisha baadhi yao, kuamua vile wanavyoona na wengine kuwasilisha malalamiko kwa viongozi wakuu.
“Nyinyi ni viongozi mliokabidhiwa dhamana kubwa katika mikoa yenu, lakini pia nyie ndio wawakilishi wa Mheshimiwa Rais katika hiyo mikoa yenu, uwajibikaji na mshikamano ndio sababu pekee itakayowezesha watanzania kutimiza wajibu wao wa kuboresha maisha yao,” alisisitiza.
Alisema maendeleo katika mikoa hiyo, kamwe haitawezekana endapo viongozi hao wa juu wa mikoa, hawatakuwa wawazi katika mawasiliano baina yao, uhusiano wao kikazi ukiwa mbaya na kukiwa na kutokuelewana.
“Mawasiliano ya katibu tawala kwenda kwa mkuu wa mkoa ni ushauri, maelezo, ufafanuzi na taarifa muhimu, wakati mawasiliano ya mkuu wa mkoa kwenda kwa katibu tawala zaidi ni maelekezo ya kisera na uwajibikaji,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, katibu tawala wa mkoa husaini na mkuu wa mkoa mkataba wa utendaji kazi, ambapo katika tathmini ya mwaka, suala la uhusiano wao ni miongoni mwa vipimo vilivyomo kwenye tathmini hiyo.
Aliwataka viongozi hao, kuepuka misuguano baina yao, ambayo huenda ikaigwa na ngazi za chini na kusababisha utendaji katika mkoa mzima kuwa mbaya na hivyo kuurudisha nyuma mkoa husika.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia, alisema Serikali siku zote imekuwa ikisisitizia viongozi wake kuthamini na kuheshimiana, lakini kubwa zaidi kuhakikisha kuwa hawaingiliani katika utendaji wao.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Joseph Semboja, alisema mafunzo hayo yamelenga katika kuwakumbusha viongozi hao juu ya umuhimu wa kuzingatia suala la mawasiliano, kuepuka kuingiliana katika utendaji na kuwa na uhusiano mzuri baina yao katika kuwatumikia wananchi.
“Tumeanza na wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa wa Tanzania Bara, tutafanya pia mafunzo kwa viongozi kama hao Zanzibar na kushuka hadi ngazi za chini kuanzia wakuu wa wilaya na watendaji, lengo ni kuimarisha mazingira mazuri ya utendaji baina yao,” alisema.

Comments

Popular Posts