Saturday, July 12, 2014

WAKILI WA SERIKALI BADO AENDELEA KUSOTA RUMANDE

Wakili  wa Serikali, Yasinter Rwechungula (44)  Mkazi wa Boko njia panda, anayekabiliwa na kesi ya kupiga na kujeruhi mwili ameendelea kusota rumande kutokana na kutotimiza masharti ya dhamana.
Hakimu wa Mahakama ya Mkazi Kinondoni,  Amaria Mushi, alimtaka kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh milioni nne.
Alishindwa kutimiza masharti hayo hivyo alirudishwa rumande hadi Julai 29 mwaka huu kesi yake itakaposikilizwa.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali Masin Musa alidai Juni 11 mwaka huu mshitakiwa alifikishwa katika Mahakama hiyo kwa  kosa la kupiga na kujeruhi mwili.
Alidai mshitakiwa alimpiga msichana wake wa kazi Malina Mathayo (15) kwa kutumia waya wa kompyuta mwilini na kumpiga na brenda kichwani na kumsababishia majeraha ya mwili.
Pia alidai Juni 17 mwaka huu , Jamhuri waliweka zuio la dhamana kwa ajili ya usalama wa mtuhumiwa, huku akidai kuwa hali ya mgonjwa mpaka sasa inaendelea vizuri.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Mushi alisema ameridhika na ufafanuzi uliotolewa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Musa pamoja na Wakili wa mshitakiwa Golden Njahara, hivyo alidai haki ya dhamana iko wazi  endapo atatimiza masharti yaliyopangwa.

No comments: