Saturday, July 19, 2014

VODACOM YAADHIMISHA SIKU YA NELSON MANDELA

Wafanyakazi Ubalozi wa Afrika Kusini nchini na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, jana waliungana na taasisi na wananchi kutoka sehemu mbalimbali duniani katika kuadhimisha Siku ya  Nelson Mandela.
Mandela alikuwa Rais wa  Kwanza mweusi wa Afrika Kusini,  aliyejitolea maisha yake kupigania na kuondoa vitendo vya ubaguzi wa rangi na unyanyasaji nchini humo.
Alifariki dunia Desemba 5, mwaka 2013 akiwa na umri wa miaka 95.
Siku ya Mandela ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuadhimishwa Julai 18 ya kila mwaka.
Taasisi mbalimbali duniani, hushiriki kufanya kazi za kujitolea kuhudumia jamii kwa muda wa dakika 67, kumuenzi kiongozi huyo aliyeleta mapinduzi makubwa yenye historia ya  kipekee duniani.
Katika kuenzi siku hiyo, Ubalozi wa Afrika Kusini nchini, Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa na    wafanyakazi wa Vodacom,  walishiriki katika shughuli za kuhudumia jamii kwa kusafisha mazingira ya shule ya watoto  wenye mahitaji maalumu ya Sinza, Dar es Salaam, ambapo pia wamegawa zawadi mbalimbali kwa watoto wanaosoma shuleni hapo.
Kaimu Balozi  wa Afrika Kusini nchini, Terry Govender alisema wanajivunia kuwa na kiongozi hodari, kama Nelson Mandela, ambaye alijitolea nusu ya maisha yake kupigana dhidi ya ubaguzi mchini Afrika Kusini.
Aliwaasa watu kufuata nyayo zake, kwani ni mfano wa kuigwa duniani.
Akizungumza juu ya kushiriki katika tukio hili, Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu alisema kuwa kampuni inaona fahari kubwa kushiriki na kutoa udhamini kwa tukio hili muhimu la siku ya kiongozi mashuhuri duniani, mwenye historia ya pekee katika mapambano ya kutokomeza vitendo vya kufifisha haki za binadamu.
“Vodacom tunajivunia kushiriki katika shughuli za kijamii za kuadhimisha siku maalumu ya kiongozi shupavu wa Afrika, hayati Nelson Mandela, aliyejitolea maisha yake yote kupambana na vitendo vya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na kuhakikisha vinatokomezwa kwa njia ya amani,”alisema Nkurlu.

No comments: