Wednesday, July 16, 2014

VIJEMBE NA MIPASHO VYATIBUA ZIARA YA WAZIRI

Ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla kukagua miradi ya maji jijini Dar es Salaam, jana iliingia dosari,  kutokana na vitendo vya baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Miradi hiyo ambayo anakagua, inatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA).
Hali hiyo ilijitokeza katika maeneo ya Shule ya Msingi Mavurunza na Kibamba Njia Panda jana.
Katika maeneo yote hayo,  wafuasi hao mara kadhaa walikatiza hotuba za viongozi waliofuatana na Makalla, kwa kuzodoana, kulumbana, kutambiana, kutoleana  kejeli, vibwagizo na maneno makali.
Hali ya hewa ilianza kuchafuka katika eneo la Shule ya Msingi Mavurunza,  ambako kulikuwa na wafuasi kadhaa wa Chadema na wa CCM.
Baadhi ya wafuasi hao, walikuwa  wamevaa sare za vyama vyao na wengine walikuwa hawana sare. Wengine walibeba vibendera vidogo huku wengine wakiwa na  bendera kubwa, ambazo walizipepea kwa fujo.
Wafuasi  hao wa Chadema walibeba mabango  kadhaa yaliyosema ‘Waziri hatutaki porojo, tunataka maji’ na ‘CCM kazi ya kuleta maji imeshindwa. Chadema Juu’.
Wafuasi wengine wa Chadema, walikuwa wakitoa vibwagizo vya ‘Maji,  Maji, Maji’ na ‘Tunataka Maji, Tunataka Maji’.
Kwa upande wao, wafuasi wa CCM walibeba mabango kadhaa, yaliyosomeka ifuatavyo:'Mnyika  kodi yako imekwisha, mwenye nyumba anataka Jimbo lake. CCM’ , ‘Hongera viongozi wa CCM kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010/2015’, ‘Mnyika tumechoka na hoja binafsi, mwongozo, tunataka hoja zetu wananchi’.
Mabango mengine yalisema,  ‘Mnyika hatukuoni hadi uletwe na Naibu Waziri Makala, njia uliyopita mwaka 2010 imeota magugu’ na ‘Mnyika uliwaahidi kinamama katika mkutano wa Vicoba vya Jimbo Sh 10,000,000 iko wapi? Huo siyo usanii’.
Alipopewa nafasi ya kuhutubia, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) aliwaita mbele waliobeba mabango hayo na yeye aliyasoma kwa sauti kubwa ili wote waliokuwepo hapo wasikie.
Baada  ya hapo, Mnyika alijaribu kujibu yaliyoandikwa kwenye mabango hayo, lakini majibu yake yalikatizwa na vibwagizo.
Hali ilikuwa hivyo hivyo hata aliposimama Makalla ili kuhutubia. Makala alijaribu kuwasihi wafuasi wa Chadema watulie, wamsikilize, lakini  utulivu haukuwepo.
Ndipo Naibu Waziri huyo aliwaeleza polisi, watulize wafuasi hao. Kuona hivyo, Mnyika alimpinga Makalla kwa kumhoji kwa nini kwanza hakuwatuliza  wafuasi wa CCM, waliokuwa wanapiga kelele. Mnyika na Makalla waliketi jirani meza kuu.
Kilichofuatia ni zogo kubwa baina ya viongozi kadhaa wa CCM na Chadema, walioketi meza kuu, ambapo baadhi yao nusura washikane mashati, kutokana na kila mmoja kutetea chama chake.
 Hali hiyo ya kutambiana na kuzodoana, ilijitokeza pia katika eneo la Kibamba Njia Panda, ambako Makalla alifanya mkutano mwingine wa hadhara.
 Akihutubia wananchi, Makalla alisisitiza kuwa serikali imepania kumaliza tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam hivi karibuni kupitia miradi kadhaa, inayotekelezwa na DAWASA.
Alieleza kuwa serikali imetenga Sh bilioni 362 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa mitambo miwili ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini. Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini pamoja na ulazaji wa bomba kubwa  kutoka Ruvu Chini hadi matangi yaliyopo Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar, utakamilika hivi karibuni.
Kwa upande wa Ruvu Juu, upanuzi wake utakamilika Agosti mwakani na ujenzi wa chujio mpya, tayari umeanza. Ulazaji wa bomba kubwa kutoka Ruvu Juu hadi Kibamba na Kimara, utaanza Septemba mwa huu.
Makalla alisema maeneo mengi ya Dar es Salaam, yana kero ya maji kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji. Alifafanua  kuwa maji yanayozalishwa na DAWASA kwa sasa ni lita milioni 300 kwa siku, wakati mahitaji ni lita milioni 450 kwa siku, hivyo kuna upungufu wa lita milioni 150 kila siku. Alisema ongezeko la mahitaji ya maji, linatokana na ongezeko kubwa la watu, uchakavu wa miundombinu na wizi wa maji.
Kwa upande wake, Mnyika alisema  kila mara  amekuwa akiitaka serikali kutatua kero ya maji katika jimbo lake hilo na kuna wakati aliwasilisha hoja binafsi bungeni  Februari 4, mwaka 2013.
Pia, alisema amekuwa akifanya ziara nyingi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, kuangalia tatizo hilo na kushauriana na wananchi jinsi ya kulitatua. Pia, alisema alishafanya ziara pamoja na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji, Binilith Mahenge.
Kabla ya Mnyika kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010, mbunge wa Ubungo alikuwa ni Charles  Keenja wa CCM. Ziara hiyo ya Makalla kukagua miradi ya maji, inaendelea. Makalla pia ni mbunge wa Jimbo la Mvomero (CCM).

No comments: