Wednesday, July 2, 2014

TRA YADALIANA NA WENYE VITUO VYA MAFUTA KUHUSU EFDS

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema iko kwenye majadiliano na wadau wa vituo vya mafuta nchini, ili kuangalia namna bora ya kufunga mashine za kieletroniki za utoaji risiti kwenye pampu za vituo hivyo.
Awali mamlaka hiyo, ilitoa agizo kwa wamiliki wa vituo hivyo kuhakikisha kuwa wamefunga mashine hizo kwenye pampu za mafuta kabla ya Juni 30.
Akizungumza na gazeti hili, Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema bado mamlaka hiyo inasimamia utaratibu huo na kwamba kwa sasa kinachoendelea ni majadiliano ya namna ya kuboresha huduma hiyo.
 “Kuna maboresho tunafanyia kazi ili kupata maarifa mapya, tutatoa maelekezo baadaye, tumeona kuwa kufunga mashine hizi ndani na nje ya pampu za mafuta kuna vitu vingi vya kufanyia kazi,” alisema Kayombo.
Alisisitiza kuwa msimamo wa TRA uko palepale kuwa lazima vituo hivyo vyote vifungiwe mfumo huo wa mashine za kieletroniki za utoaji risiti ambapo kila pampu itakapomaliza kutoa mafuta hapohapo itatoka risiti kwa mteja inayoonesha kiwango cha mafuta kilichouzwa na gharama zake.
Mfumo huo wa kutumia mashine za kodi za kielektroniki ulianza kutekelezwa kwa awamu ya kwanza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na awamu ya pili ulianza mwaka 2013 ikiwahusu wafanyabiashara wasiosajiliwa kwenye VAT na wenye mauzo ghafi kwa mwaka ya Sh milioni 14 na zaidi.

No comments: