Wednesday, July 9, 2014

PUMBA ZA MCHELE ZATUMIKA KUTENGENEZA MATOFALI

Pumba za mchele zimebainika zikichanganywa na saruji kidogo, zina uwezo wa kutengeneza matofali imara.
Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA), umebaini hayo kupitia tafiti mbalimbali ilizofanya.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa NHBR, Lyakurwa Frimin kwenye Maonesho ya 38 ya Biashara Kimataifa katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema mabaki ya viwandani na  mashambani, yanaweza kutumika kutengeneza matofali mazuri, ambayo hayahitaji gharama kubwa kutokana na matumizi ya kiwango kidogo cha saruji.
“Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wakala  zimebaini kuwa hata pumba za mchele zinaweza kutengeneza matofali kwa kuchanganya na  saruji kidogo ili kupata matofali imara,” alisema.
Alisema  wananchi pia wanaweza kutumia udongo wa mfinyanzi na saruji kidogo na kutengeneza matofali, ambayo hayahitaji  kujengewa zaidi ya kuyapanga.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, nyumba bora za bei nafuu kwa wananchi hata wa kipato cha chini, zinawezekana kuwa na nyumba bora, ambayo ni za kudumu wakitumia vifaa vya bei nafuu.
Alisema nyumba zinazojengwa kwa matofali ya bei nafuu, ambayo yanapangwa bila kujengewa, nyumba inakuwa haihitaji kiyoyozi, kutokana na hewa kupitia kwenye matundu yaliyowazi.
Alisema wakala unauza  mashine za kufyatuali matoali ya aina yote, ambayo wanauza kwa bei bora, pamoja na ya kutengeneza  mabati aina ya vigae ambayo hayahitaji kazi  kutengeneza.

No comments: