Tuesday, July 8, 2014

METL YAFAGILIWA KWA KUTOA AJIRA KWA WAKULIMA, VIWANDANI

Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa amepongeza makampuni yaliyo chini ya Kundi la METL, kwa kuhakikisha ajira kwa watanzania na soko la malighafi kwa wakulima wa bidhaa mbalimbali nchini.
Silaa alisema hayo jana alipotembelea banda la METL na kujionea bidhaa mbalimbali, zinazozalishwa na makampuni yake mbalimbali  zikiwemo bidhaa za michikichi na katani.
Alisema kwa kutengeneza sabuni, mafuta na mali ghafi nyingine kutokana na michikichi, kampuni za METL zinawezesha wakulima kujiendeleza na pia kuwa na uhakika wa soko.
METL yenye makampuni zaidi ya 25, sehemu kubwa ya bidhaa zake zinatokana na mali ghafi, inayozalishwa nchini na nyingine ni zile zinazotumika kwa ajili ya wakulima kama matrekta.
Aidha, katika banda hilo kubwa ambapo kulijaa aina mbalimbali ya bidhaa kuanzia sabuni, vitenge, mafuta ya mawese,vinywaji baridi, matrekta na bidhaa za nyumbani, Meya huyo alichezesha bahati nasibu za watu waliotembelea banda hilo.
Akizungumzia uwekezaji wa METL, Silaa alisema kwamba anafarijika na jinsi bidhaa za kampuni hizo zinavyoimarika ubora kila mwaka na kusema wakati umefika kwa serikali kuangalia wawekezaji wazawa.
Alisema kwa maoni yake, serikali ione jinsi ya kuwasaidia wawekezaji wanaoagiza mitambo toka nje ili kodi wanaoyotakiwa kulipa wailipe baada ya kuanza kazi za uzalishaji.
“Hii itasaidia sana kuwa na wawekezaji wa ndani ambao wataweza kutoa huduma kama soko la mali ghjafi na pia kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa kutoka Tanzania,” alisema Silaa.
Aidha, Silaa alipongeza MeTL Group kwa kuweza kutoa ajira kwa watanzania wazawa huku bidhaa zake nyingi zikiwa kimbilio la watanzania wote, hasa wa kipato cha chini.
“Naipongeza MeTL Group, kwa kuzalisha bidhaa bora ambazo ni kimbilio la wananchi wengi… hasa bidhaa zake za mafuta, sabuni, unga, vinywaji na bidhaa zingine kibao” alisema Silaa
Pia, aliipongeza MeTL kwa upande wa kutoa ajira na kukuza uchumi hapa nchini, ikiwemo kuzalisha bidhaa nyingi na zenye ubora, ikiwemo za kamba ya mkonge, ambayo alisema ni majibu ya utunzaji wa mazingira kutokana na vifungashio vya plastiki kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Katika bahati nasibu iliyochezeshwa,  mkazi wa Kijitonyama Jijiji Dar es Salaam, Irene Manamba amejishindia zawadi ya pikipiki mpya.
Aidha, katika droo hiyo, washindi wengine waliojishindia zawadi mbalimbali katika droo hiyo majina yao na wanakotoka ni  Victoria Charles  ambaye alikuwa mshindi wa pili  mkazi wa Temeke, Julius Kamele (Tabata),  Irene Mushi (Kijitonyama),  Semi Anderson ((Dar es Salaam), Happyness Kalokola (Kitunda), Noel Kalenga (Sinza Kumekucha), Adam  Mkwaya (Mabibo), Mery  Msangi (Dar es Salaam) na Aisha Abeid (Tabata).
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni  ya MeTL GROUP, Fatema Dewji- Jaffer  alieleza kuwa  droo hiyo ni maalumu kwa ajili ya wateja wote waliopata kutembelea  banda hilo tokea siku ya kwanza na kujiorodhesha majina yao.
Fatema alisema MeTL Group imeamua kutoa zawadi  hizo, kama shukrani  na kujitangaza zaidi kwa wateja na wananchi waliopata kutembelea na kununua bidhaa  za MeTL Group.
“Kwa ubora wa bidhaa zetu za MeTL Group,  kama  inavyojulikana  ‘The People’s  Brand’,   kwa droo hii wateja wetu watafurahia  kwa zawadi hizo nono,” alisema Fatema.
 Aidha, MeTL Group  imetambulisha rasmi vinywaji  vyake vipya kwenye maonyesho hayo ya Saba Saba, ikiwemo vinywaji vinapendwa na wengi kwenye maonyesho hayo, MO Cola,  MO Portello na MO Malt.  Vingine ni  MO  Lemon Mint,  MO chungwa na MO Bomba.

No comments: