MABOMU YATUMIKA KUZIMA VURUGU KANISA LA MORAVIAN

Jeshi la Polisi jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi, kutawanya waumini wa Kanisa la Moravian Ushirika wa Kinondoni, baada ya makundi mawili yanayovutana, kuibua vurugu kanisani hapo.
Waumini na viongozi wa kanisa hilo 29 wanashikiliwa na polisi, kutokana na tukio hili.
Kabla ya polisi kuchukua hatua ya kupiga mabomu ya machozi, kundi moja linalosali sehemu ya juu ya kanisa, liliingia kanisani humo tangu juzi alasiri, huku kundi linaloendesha ibada yao chini, wakitaka watu hao waondoke.
Pande hizo ziliendelea na mvutano usiku kucha mpaka jana asubuhi vurugu hizo zilipozidi, kutokana na baadhi ya wafuasi wa kundi linalosali chini, kuzuia waliokuwa juu kupelekewa chakula. Mvutano huo ulisababisha vyakula kumwaga.
Saa 1:50 asubuhi gazeti hili lilishuhudia Polisi wakiwasili eneo la kanisa hilo na kutuliza vurugu hizo. Lakini baada ya muda, liliingia gari lililobeba waumini wanaosadikiwa kutoka kanisa lingine la Mabibo, hali iliyoibua upya vurugu.
Baada ya Polisi kushindwa kutuliza vurugu hizo kwa amani, walilazimika kupiga mabomu ya machozi na kuwakamata baadhi ya viongozi na waumini wa kanisa hilo bila kujali upande, huku wengine wakikimbia.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alithibitisha kuwa wanawashikilia watu 29 kwa mahojiano.
“Mimi sijui kama ni waumini au viongozi, ninachujua tumewakamata wafanya fujo 29. Kwa sasa tunawahoji…. kesho (leo) tutayapeleka majina kwa mwendesha mashtaka wa serikali ambaye ataamua sheria za kuwachukulia,” alisema Wambura.
Kabla ya kupigwa mabomu na kukamatwa watu hao, Mchungaji wa kundi linalosali chini, James Mwakalile alisema upande mwingine ulivunja mlango na kuingia kanisani kinyume cha utaratibu.
“Kwa miezi sita hatuna raha na amani kila ifikapo jumamosi na jumapili, tunaomba serikali ilichukue hatua za haraka kumaliza matatizo yao,” alisema mmoja wa majirani wa eneo hilo, Mwanaharusi Salum.

Comments

Popular Posts