Tuesday, July 8, 2014

HOSPITALI YA MKOA INA DAKTARI BINGWA MMOJA TU

Hospitali ya  Rufaa ya mkoa wa Kagera inakabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa saba, hali inayotajwa kuchangia huduma kusuasua hivyo  kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa wagonjwa.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Juma Nyakina alisema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini hapa, juu ya  changamoto zinazoikumba hospitali hiyo.
Dk Nyakina alisema  wagonjwa wamekuwa wakilalamikia huduma mbovu hususani kukaa muda mrefu bila kupata huduma kutoka kwa madaktari kutokana na foleni.
“Kweli tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa lakini naomba mtambue kwamba tuna upungufu mkubwa wa madaktari bingwa ukiangalia hospitali hii ni ya mkoa, lakini ina daktari bingwa mmoja tu ambapo mahitaji ni wanane,” alisema.
Aliendelea kusema, “hivi sasa watoto walio wengi hawachukui masomo ya sayansi kwa hiyo madaktari watatoka wapi?.”
Kwa mujibu wa mganga huyo, wodi ya wazazi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watoa huduma ambapo wako 13 badala ya 24,  jambo ambalo linasababisha mhudumu akihudumia wagonjwa wengi kupita uwezo.
“Unakuta mhudumu mmoja anahudumia wazazi watano hadi 20 kwa zamu ya asubuhi mpaka saa saba wakati kisheria anapaswa kuhudumia mgonjwa mmoja hadi wawili kwa zamu moja,”aliongeza.
 Aidha alisema ukosefu wa  madaktari bingwa na watoa huduma wengine, unaleta  changamoto hata kwenye utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaohudumiwa na Mfumo wa Bima ya Afya.
Alisema ingawa wana dirisha lao, lakini  akihitajika daktari bingwa, huyo huyo anapaswa ahudumie wagonjwa wengine.

No comments: