Monday, July 7, 2014

'FEDHA KWENYE ASASI ZILIZO CHINI YA BENKI KUU NI SALAMA'

Wananchi wameshauriwa kujenga utamaduni wa kuweka akiba katika benki na taasisi za fedha zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kile kilichoelezwa ni njia salama na yenye faida kwao na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,  Meneja wa Fedha na Utawala wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Richard Malisa, alisema amana zinazowekwa na wateja katika benki na taasisi za fedha, zinatoa fursa kwa vyombo hivyo vya fedha, kuwa na uwezo mkubwa wa kukopesha kampuni na wafanyabiashara mitaji ya kuendeshea shughuli zao.
“Umuhimu wa benki katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi ni sawa na umuhimu wa injini kwenye gari, kwani hufanya kazi kubwa ya kuunganisha pamoja mahitaji ya wenye kutaka kupata mahali salama pa kutunza fedha zao kwa faida na wale wenye mahitaji ya kupata mitaji kuendeleza shughuli zao za kiuchumi,” alisema Malisa.
Aliwatoa wasiwasi kuhusu suala la usalama wa fedha zao na kusisitiza kuwa madhumuni ya taasisi hiyo ni kuhakikisha kuwa inalinda kwa mujibu wa sheria amana zao katika vyombo vya fedha vilivyopewa leseni ya biashara na BoT.
Meneja wa Uendeshaji wa chombo hicho, Rosemary Tenga, alisema taasisi hiyo ina jukumu la kukusanya michango kutoka kwa wanachama wake ambao ni benki na taasisi zote za fedha zilizopewa leseni na BoT kwa madhumuni ya kendelea kutunisha Mfuko wa Bima ya Amana.
Pia alisema taasisi hiyo ina wajibu wa kuwekeza kwenye dhamana za Serikali fedha zinazokusanywa kama michango kutoka kwa wanachama na faida inayopatikana kwenye uwekezaji huu huwa ni chanzo kimojawapo cha mapato ya taasisi hiyo.

No comments: