Tuesday, July 15, 2014

DAR YATOA SHILINGI MILIONI 7 KWA WAJASIRIAMALI

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Mipango Miji imetoa Sh milioni saba, kama mikopo kwa vikundi vitatu vya wajasiriamali.
Hayo yalisemwa na Ofisa Maendeleo wa Jiji, Magreth Mazwile wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi hivyo jijini.
Alisema kuwa lengo la kuwapatia mkopo huo ni kuwasaidia wajasiriamali katika kuongeza mtaji na kujikomboa na hali ngumu ya maisha.
Kundi la kwanza la wajasiriamali lijulikanalo kama Mindu Youth Group chenye wanachama tisa, walikabidhiwa Sh milioni mbili kwa ajili ya kuongeza mtaji ambazo shughuli kubwa za kundi hilo ni ufundi seremala, kutengeneza thamani za majumbani na ofisini.
Aliongeza kuwa kundi la pili kutoka Buguruni Kisiwani, la Hygiene and Technician Environment Group lenye wanachama 20  limepatiwa mkopo wa Sh milioni 2.5 ambazo zitawasaidia katika shughuli mbalimbali za usafi wa mazingira, kununua mikokoteni 20 na vifaa mbalimbali vya ofisi.
Aidha, alisema kundi la tatu kunufaika na mkopo huo Vicoba Tunaweza Group A ambalo lina wanachama 25 na walipatiwa Sh milioni 2.5, shughuli kubwa zinazofanywa na kundi hilo ni mradi wa uuzaji wa vyakula vya nafaka.
Naibu Meya wa Jiji, Zena Mgaya ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka wajasiriamali hao kurejesha mikopo hiyo kwa wakati kama walivyopangiwa ili waweze kuwasaidia wajasiriamali wengine akibainisha kuwa huo ni mwanzo tu na wangehitaji kuendelea kuwasaidia wajasiriamali wengine.

No comments: