Saturday, July 12, 2014

BENKI YA DUNIA YASAIDIA ELIMU KUPITIA BRN

Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia (WB) imeidhinisha Dola za Kimarekani milioni 112 kwa ajili ya kuisaidia Tanzania kuimarisha sekta ya elimu kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Tanzania, Philippe Dongier, alisema pamoja na msaada huo, benki hiyo pia imeidhinisha msaada wa kuimarisha Sekta ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia kwenye elimu ya juu, lengo likiwa ni kuzalisha wataalamu wengi zaidi ambao wataweza kuendana na mahitaji ya uchumi wa sasa.
Akizungumzia msaada huo wa kuimarisha sekta ya elimu kupitia BRN, Dongier alisema takribani  muongo mmoja sasa, zaidi ya watoto milioni moja wenye umri wa kuanza shule nchini  waliandikishwa na kwamba jambo muhimu hivi sasa ni kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.
Alisema Benki ya Dunia imeanzisha programu mpya ambayo inaangalia matokeo ya sekta mbalimbali na kwa mara ya kwanza inasaidia sekta ya elimu nchini ambapo fedha hizo zinatumika kwa miaka minne kuanzia sasa.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Masuala ya Elimu wa Benki hiyo, Arun Joshi alisema  kupitia programu hiyo  mpya ya elimu kutoka Benki ya Dunia, Tanzania ambayo ni mshirika wake itafaidika  kwa kuhakikisha watoto wa shule za msingi na sekondari wanasoma kwenye mazingira bora.
Katika mpango wa pili wa kuimarisha elimu ya sayansi na Teknolojia, alisema dola  za Marekani milioni 15 zitatolewa ili kuimarisha eneo hilo.
Alisema kila mwaka watu 800,000 huingia kwenye soko la ajira na wengi wao wakiwa na upungufu wa ujuzi hivyo kufanya wakose ajira na kwamba mpango huo umelenga kuimarisha uwezo wa nguvukazi hiyo ili waweze kuingia sokoni na kushinda kwa kuwa watakuwa na uwezo na ujuzi.

No comments: