Baada ya miaka 30 ya kuishi bila ya ndoa, Rais
mpya wa Malawi, Profesa Peter Mutharika, hatimaye amefunga pingu za maisha na
mbunge wa zamani wa Jimbo la Balaka, Gertrude Maseko.
Kabla ya ndoa yao iliyofungwa jana kwenye
Kanisa la Mtakatifu Michael na Malaika Wote jijini Blantyre, Maseko aliwahi
kuolewa, lakini ndoa yake ilivunjika miaka kumi iliyopita; na mwaka jana mume
wake huyo, ambaye pia alizaa naye mtoto mmoja, anayesoma Chuo Kikuu, aliaga
dunia.
Aidha, kwa Rais Mutharika, Profesa aliyebobea
katika masuala ya sheria, aliwahi kumwoa Christophine G. Mutharika, raia wa
Visiwa vya Carribean. Alibahatika kuzaa naye watoto watatu, Mahopela ambaye ni
wa kiume na mabinti, Monique na Moyenda, ambao wote ni wanasheria mahiri nchini
Marekani kwa sasa.
Hata hivyo, Mutharika alimpoteza mkewe huyo
kwa ugonjwa wa kansa mwaka 1990, hivyo kumfanya asioe kwa muda mrefu, huku
akijikita zaidi katika kazi zake za uwakili kwa zaidi ya miaka 40 nchini
Marekani.
Katika ndoa iliyoongozwa na Padri Rapson
Chikwenzule, Rais Mutharika hakuwa na mbwembwe nyingi kama mkuu wa nchi na
alitarajiwa kuendelea na sherehe katika shamba la familia ya Rais huyo lililopo
Ndata Wilaya ya Thloyo, Kusini mwa Malawi.
Ukiondoa makundi ya marafiki na wageni
waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi, miongoni mwa walioshuhudia wawili hao
wakioana ni mabinti wa Mutharika, ambao walikanyaga ardhi ya Malawi kwa mara ya
kwanza baada ya baba yao kuutwaa urais wa Malawi Juni Mosi, mwaka huu.
Kaka yao ambaye pia ni profesa katika moja ya
vyuo vikuu vya Marekani, hakuhudhuria na hajawahi kukanyaga nchi ya Malawi.
Hata hivyo, ujio wa watoto hao umemaliza
uvumi, uliokuwa umeenezwa wakati wa kampeni za urais, kwamba Mutharika si
mwanamume aliyekamilika na hajawahi kuwa na watoto.
Akizungumza siku moja kabla ya harusi hiyo,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Harusi ya Rais Mutharika na Maseko,
Saulos Chilima ambaye ni Makamu wa Rais wa Malawi, alisema harusi ya `bosi’
wake ilitarajiwa kugharimu dola za Kimarekani 95,000 (Sh milioni 155).
Alisisitiza kuwa fedha hizo si za Serikali,
bali ni michango kutoka kwa pande mbili za maharusi, hasa ndugu na marafiki.
“Kila kitu kimekwenda sawa, nashukuru dhamira
ya kutogusa fedha za Serikali imetimia. Michango imetoka kwa ndugu na marafiki.
Kuna watu waliotaka kutumia mwanya wa harusi kujiweka karibu na Rais au
wasaidizi wake, hawa ‘tuliwafungia vioo’. Hatukutaka baadaye waje kutusumbua
wakitaka kusaidia kufanikisha mambo yao kwa kigezo cha ukaribu na Rais na hasa
kwa kushiriki kikamilifu katika harusi yake. Hilo tumesema hapana, hatutaki
rushwa na tutapambana kwa dhati na rushwa na wala rushwa,” alisema Chilima.
Mutharika (74) ambaye ni Rais wa Tano wa
Malawi, anakuwa Rais wa tatu kuoa akiwa madarakani. Wa kwanza kuoa akiwa Ikulu,
alikuwa Bakili Muluzi ambaye baada ya kuachana na Anne, alimwoa Shanil
Dzimbili.
Baadaye, Bingu wa Mutharika, Rais wa Tatu
ambaye ni kaka wa Rais wa sasa, yeye alimwoa Callista Mutharika baada ya kufiwa
na mkewe, Ethel.
Marais wengine waliowahi kuitawala Malawi ni
Dk Hastings Kamuzu Banda ambaye alikuwa Rais wa Kwanza wa Malawi na Joyce
Banda, Rais wa Nne ambaye ameangushwa na Profesa Mutharika katika uchaguzi mkuu
uliofanyika Mei 20, mwaka huu.

No comments:
Post a Comment