Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imetangaza mpango wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura ili kuruhusu
Watanzania wenye sifa kujiandikisha upya, viongozi wa dini nchini wameitaka
tume hiyo kubadilisha pia siku ya kupiga kura, kutoka siku ya Jumapili ambayo
huwa ya ibada hadi siku ya katikati ya wiki.
Aidha, wameshauri siku itakayochaguliwa
kwa ajili ya kupiga kura, itangazwe kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa fursa
kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchakato wa kupata viongozi wa ngazi
mbalimbali nchini kwa njia ya kidemokrasia.
Ushauri huo ulitolewa jana katika mkutano
wa viongozi wa dini na NEC kwa ajili ya kuwashirikisha viongozi hao kuhamasisha
waumini wao kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura
unaotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.
Walisema kwa kufanya uchaguzi siku isiyo
ya ibada, itawezesha waumini wengi kujitokeza kupiga kura.
Mchungaji Benard Kingo wa Kanisa la EAGT
alisema ni vema kuangalia siku hiyo ya kupiga kura, isiingiliane na siku ya
ibada. Alisema ni vema kuiweka katikati ya wiki, hivyo kusaidia kuongeza idadi
ya wapigakura.
Mwenyekiti wa Tume, Jaji mstaafu Damian
Lubuva alikubali kupokea ushauri huo na kueleza bayana kuwa kufanya uchaguzi
siku za ibada imekuwa ni mazoea.
Lakini, alisema katika baadhi ya nchi
walizotembelea, wamekuwa wakifanya uchaguzi katikati ya wiki na kufanya siku ya
mapumziko.
Aidha, baadhi ya viongozi hao wameishauri
Tume kutotumia walimu katika kuboresha Daftari hilo au kusimamia upigaji kura,
bali wawatumie wasomi katika maeneo husika, ambao hawana ajira.
Ushauri huo ulitolewa na Mchungaji Aguttu
Oballa wa Kanisa la Mennonite Sinza,
aliyeeleza kuwa walimu hao tayari wako kwenye ajira, lakini wapo wasomi wengi
katika maeneo husika wa kidato cha sita hata chuo kikuu, ambao wangesaidia
kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
“Kutokana na ukubwa wa suala hili na
kuhamasisha watu wengi kujitokeza ni vema mkawaangalia wasomi waliopo mitaani,
kusaidia kwa kuwapa ajira hiyo ya muda ili kuongeza kipato na siyo kuwatumia
walimu mara zote ambao tayari wako kwenye ajira,” alisema.
Shekhe kutoka Baraza la Waislamu Tanzania
(BAKWATA), Mohammed Said aliishauri Tume kutumia wasomi ambao watakuwa makini,
kwa kutowasumbua Waislamu kutoa kofia na hijabu wakati wa upigaji kura, kama
ilivyoagizwa na tume hiyo.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni
waumini wengi wa dini hiyo, wameshindwa kujitokeza kujiandikisha kupiga kura,
kutokana na kutakiwa kutoa kofia au hijabu, jambo wanaloamini linakwenda
kinyume na imani ya dini yao.
Akizungumzia suala hilo, Kamishna wa Tume
hiyo Zanzibar, Mchanga Hassan Mjaka alisema kinachotakiwa katika picha ni sura
ya mtu, hivyo haitakiwa waumini kutolewa mavazi hayo, isipokuwa wale wanaovaa
mavazi ya kufunika uso na kuacha macho ndiyo watatakiwa kuvua. Alibainisha kuwa
kwa mwaka huu, hatarajii suala hilo kutokea, kwani watawaelimisha watendaji.
Mratibu wa Baraza la Maaskofu wa
Kikatoliki (TEC), Paulo Chilewa akiitaka NEC kuangalia namna ya kuhakikisha
wanafunzi katika vyuo, wanaweza kupiga kura kwa kuandikishwa maeneo
watakayokuwepo wakati wa kupiga kura.
Alisema katika uchaguzi uliopita,
walibaini wanafunzi wa vyuo zaidi ya 100,000 walishindwa kupiga kura, kutokana
na kujiandikisha vyuoni na wakati wa kupiga kura walikuwa katika majimbo yao.
Akizungumzia suala hilo, Lubuva
aliwashauri wanafunzi hao kuhakikisha wanakumbushana kufanya utaratibu wa kubadilisha maeneo
watakayokuwepo ili waweze kupiga kura.
Chilewa pia aliishauri NEC, kuongeza muda
wa kujiandikisha katika daftari la wapigakura kuishia saa 12 jioni na sio saa
tisa kama ilivyokuwa kwa vitambulisho vya taifa kuwawezesha wafanyakazi
kushiriki baada ya kutoka kazini.
Awali, akifungua mkutano huo, Lubuva
alisema viongozi hao wa dini watasaidia kuhamasisha waumini wao ambao ndio
wapigakura, kujiandikisha katika daftari hilo la wapigakura ili kuongeza idadi
ya wapigakura wenye sifa.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba
alisema kwa kutumia viongozi hao walio karibu na wananchi kutasaidia kupeleka
taarifa kwa urahisi na imani kubwa kwa wananchi wengi kwa wakati mmoja.
Uboreshaji wa daftari hilo la kupiga kura
unatarajia kufanyika Septemba kwa Watanzania wote kujiandikisha upya na kupata
vitambulisho vipya.
Hatua hiyo itasaidia kuondoa manung’uniko
ya baadhi ya wanasiasa, wanaochukulia kushuka kwa idadi ya wapigakura nchini,
kuwa kunatokana na wengi kunyimwa fursa ya kuandikishwa, wanayostahili kuipata.

No comments:
Post a Comment