Mabadiliko ya tabia nchi yameathiri visiwa vya
Zanzibar na kutishia ustawi wa kilimo hususani cha mpunga.
Waziri wa Maji, Ujenzi na Nishati, Ramadhan
Abdalla Shaaban alisema hayo jana akisisitiza kwamba kilimo cha kutegemea mvua
kimeathirika kwa kiwango kikubwa na mapato ya wakulima kushuka.
Shaaban kwa niaba ya Waziri wa Kilimo na
Maliasili, alikuwa akifanya majumuisho na kujibu hoja mbali mbali za
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia bajeti ya wizara hiyo
kwa mwaka wa fedha 2014-2015.
Alisema maeneo mengi ya kisiwa cha Unguja na
Pemba yameathirika kwa kuingia maji ya chumvi katika mabonde. Kwa mujibu
wake, zaidi ya maeneo 30 yameathirika kwa kuingiwa na maji ya chumvi
kisiwani Pemba, wakati kwa upande wa Unguja maeneo 20 yameathirika.
“Kilimo cha mpunga kwa sasa kinakabiliwa na
changamoto mbali mbali ikiwemo maji ya chumvi kuvamia mabonde ya wakulima na
kuacha moja kwa moja kilimo hicho,” alisema.
Mwakilishi wa Mtambwe, Salim Abdalla
Hamadi (CUF) alitaka serikali kuchukua hatua za haraka kukabili
mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo athari zake katika sekta ya kilimo ni kubwa.
Alitoa mfano wa jimbo lake, zaidi ya maeneo
sita yameathirika na kazi za kilimo zimesita kutokana na mwingiliano huo wa
maji ya chumvi.
“Tunaiomba Wizara ya Kilimo na Maliasili
kutusaidia kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia ya nchi,” alisema
Hamadi.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepitisha makadirio
ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo iliyoomba kuidhinishiwa Sh
13,758,000,000 kwa kazi za kawaida, mwaka wa fedha 2014/15.

No comments:
Post a Comment