Aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakati huo FAT, Kanali mstaafu
Ali Hassan Mwanakatwe amefariki dunia.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Shirikisho hilo jana kwa vyombo vya habari, Kanali
Mwanakatwe alifariki jana asubuhi kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini
Dar es Salaam.
“Kwa
mujibu wa binti wa marehemu, Sophia, baba yake alianguka bafuni nyumbani kwake
Mbezi Beach ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Lugalo ambapo ndipo umauti
ulipomfika wakati madaktari wakimpatia matibabu,” ilieleza taarifa ya Ofisa
Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura.
Kanali
Mwanakatwe alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania
(FAT) katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha mkoani Pwani.
Baada
ya kuondoka FAT, aligombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka
1997.
“Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla kwani,
Kanali Mwanakatwe enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi, na
mkufunzi wa utawala wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi
kuwa Kamishna wa CAF,” alieleza Wambura.
“TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la
Ulinzi Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.”
Kwa
mujibu wa Wambura, taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake
nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na Hoteli ya Giraffe wakati ndugu
wakisubiriwa kutoka mikoani.
Kifo
cha Kanali Mwanakatwe kimetokea siku moja baada ya Tanzania kumpoteza mchezaji
wake wa zamani wa Taifa Stars na timu za Simba na Sigara, Gabriel ‘Gebo’ Peter
aliyefariki dunia juzi.
Gebo
(53), ambaye anatoka katika familia ya soka,
ndugu zake ni wanasoka Peter Tino na Emma Peter alitarajiwa kuzikwa jana
jioni katika makaburi ya Kigurunyembe mkoani Morogoro.
Aliagwa jana nyumbani kwake Vingunguti jijini
Dar es Salaam katika shughuli ambayo ilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Ufundi
wa TFF, Salum Madadi na mtangulizi wake, Sunday Kayuni aliyekuwa kocha wake
wakati akiichezea Sigara iliyokuwa na makazi yake Chang’ombe, Temeke.
No comments:
Post a Comment