Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
ametetea umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, akisema ni jambo kubwa lenye
manufaa ambalo moja ya faida zake ni kuhimiza umuhimu wa kujitolea miongoni mwa
wananchi katika kujiletea maendeleo yao.
Aidha, Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia amesema mbio za Mwenge
zinaeneza ujumbe wenye manufaa kwa jamii, kuliko mikutano inayofanywa na kundi
linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Waziri Mkuu Pinda
alishangazwa na mjadala ulioibuliwa na wabunge wa upinzani bungeni jana kuona
Mwenge kama suala lisilo na maana kwa taifa.
“Nimesimama kwa sababu
nimesikiliza mjadala hapa, naona jambo hili kubwa, linaonekana kama halina
maana kwa taifa,” alisema Pinda na kuongeza:“Kila mwaka, mbio za Mwenge huwa na
kaulimbiu mahsusi kwa sababu Mwenge huu huwa na fursa ya kufika maeneo mengi
hivyo kufikisha ujumbe kuhusu masuala mazito ya nchi kama elimu. Kwa hiyo, si
sahihi kabisa kuona Mwenge hauna maana.”
Alisema anafahamu kuwa
wapinzani wanaweza wasipendezwe sana na Mwenge kuhimiza suala la kujitolea
miongoni mwa wananchi.
“Hili linaweza
lisiwapendeze sana wenzetu wa upande wa pili. Mwenge unahimiza suala la
kujitolea katika shughuli zao za maendeleo.
“Wananchi wanahimizwa
kuenzi moyo huo na wamekuwa wakifanya hivyo katika shughuli mbalimbali za
kijamii. Hili halina ukakasi hata kidogo.
“Hoja hapa imekuwa ni
michango, lakini hivi Mwenge unakuja pale kwangu Kibaoni, kwa ugeni huo,
unaofanya kazi nzuri, kama watu wanachanga kuku, bata, hii siyo dhambi.
Wananchi wamekuwa wakarimu sana katika jambo hili,” alisema Waziri Mkuu Pinda.
Katika swali la msingi,
Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema), alitaka kufahamu ni kiasi gani
cha fedha hutumika kwa kila wilaya kwa ajili ya mbio za Mwenge, gharama za
kuuwasha na kuuzima na faida zinazopatikana.
Akijibu swali hilo, Naibu
Waziri Nkamia alisema Serikali hutenga fedha kulingana na mahitaji ya gharama
halisi ya wakati husika.
Alitoa mfano wa mwaka
2012, Sh milioni 650 zilitengwa kwa ajili ya kuadhimisha uzinduzi na kilele cha
mbio za Mwenge wa Uhuru; ambazo kati ya hizo, Sh milioni 450 zilitumika na
Wizara na Sh milioni 200 zilitumika na mkoa mwenyeji wa kilele cha mbio hizo.
Kuhusu faida, alitaja
kuwa ni kuendelea kutunza historia na falsafa ya ukombozi wa taifa, kuhamasisha
wananchi kuhusu umuhimu wa kuendelea kuenzi amani, mshikamano, upendo na zaidi
kupambana na aina yoyote ile ya kuwabagua Watanzania kwa rangi, dini au
makabila yao.
Pia kuendelea kuhamasisha
kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kujiletea maendeleo.
Hata hivyo katika maswali
ya nyongeza, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema Mwenge unaongeza
ugumu wa maisha kwa kuchangisha wananchi na kuwa viongozi wa mbio hizo mwaka
huu wanapita kupiga propaganda ya serikali mbili na kutaka mbio hizo zifutwe.
Akijibu swali hilo,
Nkamia alisisitiza kuwa Serikali haiko tayari kusitisha mbio hizo, kwani
wananchi wana imani nazo na zimesaidia kudumisha umoja na amani. Alisema Mwenge
unatoa ujumbe mzuri kuliko unaotolewa na Ukawa.
Mbali ya Mnyika, Mbunge
wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), alihoji sababu za walimu
kulazimishwa kuchangia mbio hizo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera,Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema michango hiyo ni
hiari na hakuna anayelazimishwa kuchangia, na kwamba hailipii mafuta ya Mwenge
wala posho za wakimbizaji.
Kwa upande wake, Mbunge
wa Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM), yeye aliitaka Wizara iongeze siku za
kukimbizwa Mwenge wilayani Kishapu kwani una manufaa makubwa, na Wizara
imeahidi kulifanyia kazi ombi hilo huku ikipongeza hatua hiyo.
Baada ya hapo, Waziri
Mkuu alitoa ufafanuzi zaidi, lakini baada ya Kipindi cha Maswali na Majibu,
wabunge wa upinzani walisimama tena na kuomba Mwongozo kuhusu majibu hayo ya
mawaziri.
Waliosimama ni Mbunge wa
Nyamagana, Ezekiah Wenje (Chadema), Moses Machali (NCCR-Mageuzi – Kasulu Mjini)
na Susan Kiwanga (Viti Maalumu – Chadema), wote wakieleza kuwa wananchi
wanachangishwa, na baadhi yao kusoma ujumbe waliotumiwa katika simu zao za
mkononi.
Naibu Spika Ndugai
alisema atatoa majibu ya miongozo hiyo ‘mbele ya safari.’

No comments:
Post a Comment