Serikali imemtaka Balozi wa Uingereza nchini, Dianna
Malrose ajipime kama anafaa kuendelea kuiwakilisha nchi yake, na kuagiza nchi
yake kumwondoa mara moja.
Ametakiwa afike mara moja katika Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, kujieleza.
Anatuhumiwa kuihujumu Tanzania kwa kushiriki katika
vitendo kinyume cha maadili na Mkataba wa Vienna kuhusu masuala ya
kidiplomasia.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele
alitangaza hayo jana bungeni wakati alipochangia hoja ya bajeti ya mwaka
2014/15 ya wizara hiyo.
Kwa mujibu wa Masele, Balozi huyo amekuwa akifanya
vitendo vya kuongoza vikao vya kuihujumu Tanzania kutokana na suala la IPTL.
“Kuna ushahidi kuwa amekuwa akiendesha vikao mbalimbali
Dar es Salaam na Dodoma. Upo ushahidi wa vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume
cha maadili,” alisema.
Alisema balozi huyo amekuwa akishinikiza nchi wahisani wa
maendeleo kukataa kuipa Tanzania fedha za maendeleo kutokana na suala hilo.
Alisema balozi huyo amekuwa wakala wa Benki ya Standard
Chartered, kwa kutaka Serikali ya Tanzania ilipe fedha kutokana na mgogoro wa
kampuni binafsi.
“Ni aibu kwa Serikali ya Uingereza ya Waziri Mkuu David
Cameroon kwa Balozi wake kufanya uwakala wa Benki ya Standard Chartered
kuishawishi Serikali ikope fedha ili kulipa madeni ya kampuni binafsi, jambo
ambalo Rais amelikataa kwa nguvu zote.
“Tunampongeza Mheshimiwa Rais Kikwete kwa msimamo wa
kizalendo na kuipenda nchi yake,” alisema Masele na kuongeza: “Chini ya Mkataba
wa Vienna, huu ni uchochezi, kuvuruga amani na kutoheshimu nchi nyingine na
kufanya ujasusi,” alisema Masele na kuongeza:
“Serikali inamtaka ajipime kama anafaa kuendelea
kuiongoza nchi yake. Uingereza inapaswa kumchukulia hatua. Serikali inamtaka
afike katika Wizara ya Mambo ya Nje mara moja.
“Tunaitaka Serikali ya Uingereza ichunguze tuhuma hizi
dhidi ya Balozi wake na ichukue hatua mara moja ili kuepuka madhara zaidi ya
kidiplomasia yanayoweza kukuzwa zaidi kwa kuwepo kwa Balozi huyo.”
Alisema suala la IPTL ni lazima taratibu zifuatwe na
kwamba haiwezekani kulipia kampuni binafsi, na kuwa Tanzania inapaswa
kuheshimiwa.
“Tanzania ni nchi huru, lazima iheshimiwe, na hatutasita
kuchukua hatua kwa yeyote anayekwenda kinyume na utaratibu na sheria,”
aliongeza Masele.
Naibu Waziri amekuwa akiishawishi Marekani kukatiza
misaada yake kwa Tanzania, hivyo kutaka kuidhoofisha nchi kiuchumi.
Alisema Marekani ina miradi mingi ya maendeleo nchini,
ikiwamo ujenzi wa barabara katika mikoa kadhaa, ikiwamo Tanga, Ruvuma na Zanzibar.
Kauli yake imekuja baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini,
David Kafulila (NCCR –Mageuzi), kudai katika mchango wake bungeni asubuhi kuwa
Balozi huyo amekuwa mstari wa mbele kutaka ukweli wa IPTL.

No comments:
Post a Comment