Ugonjwa wa homa ya dengue
umeanza kusambaa kwa kasi mikoani ambapo sasa wagonjwa wapya 50 wamegundulika
huku ikielezwa wengi ni waliotoka nao mkoani Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa jana mjini
hapa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya na Dharura, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii Dk Elias Kessy.
Alikuwa akitoa taarifa
kwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven Kebwe wakati wa
kufunguliwa mafunzo kwa Waganga Wafawidhi wa Mikoa, Maofisa Afya, Wauguzi Wakuu
wa Mikoa yote ya Tanzania yenye lengo la kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo.
Alisema mpaka sasa
wagonjwa wapya 50 wamegundulika katika mikoa kadhaa nchini ambapo asilimia
kubwa ya watu hao walikuwa wamesafiri kutoka jijini Dar es Salaam na kuingia na
ugonjwa huo kwenye mikoa waliyokwenda.
Alisema tangu
ugonjwa huo uanze Januari mwaka huu zaidi ya watu 850 wameugua na wagonjwa
wanne kati yao walipoteza maisha. Alisema jitihada zinaendelea kudhibiti kuenea
kwa ugonjwa huo.
Alisema bado tatizo hilo
ni kubwa na utafiti unaendelea na Wizara kwa kushirikiana na Bohari Kuu
ya Madawa (MSD), wamekuwa wakisambaza vifaa na dawa kwenye maeneo mengi nchini.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Afya alisema ugonjwa huo ni mpya katika ukanda wa joto.
Alisema ni muhimu kujipanga kuhakikisha ugonjwa huo hauenei kama ilivyo
sasa.
Alisema kazi ni kubwa
iliyofanyika katika kutibu wagonjwa waliogundulika lakini jambo la muhimu ni
kuangalia suala zima la usafi wa mazingira.
“Tumekubaliana kupita
nchi nzima kuangalia suala la usafi wa mazingira linapewa kipaumbele, maeneo
mengi yamekuwa na nyasi, madimbwi na hata matairi ambayo kwa kiasi kikubwa
yamekuwa mazalia makubwa ya mbu kutokana na maji kutuama humo kwa muda mrefu,”
alisema.
Alitaka wataalamu hao wa
afya kusimamia vizuri suala la usafi wa mazingira na kuachana na tabia ya
kufanya kazi kwa mazoea.
“Tiba pekee ya homa ya
dengue ni usafi wa mazingira, wataalamu kwenye halmashauri walione hilo, tatizo
hili liko mbele yetu tukiligeuza kuwa malaria ya pili litakuwa tatizo
kubwa sana,” alisema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma Dk Ezekiel Mpuya alisema hospitali ya mkoa ilipata kesi moja ya
mtu aliyekuwa akiugua ugonjwa huo.
“Huyo aliyeugua alikuwa
amekwenda Dar es Salaam kikazi na aliporudi akaanza kuumwa na kulazwa lakini
alitibiwa na kupona na sasa hakuna mgonjwa tena hapa Dodoma,” alisema.
Washiriki zaidi ya 70 wanahudhuria mafunzo hayo.
Ugonjwa huo unaotokana na
kirusi kinachosambazwa na mbu aina ya Aedes , unatajwa kuwa ni wa ukanda
wa joto.
Dalili za ugonjwa huo ni
homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu huku wakati mwingine, dalili
zake zikifanana na za malaria.
Taarifa iliyotolewa hivi
karibuni bungeni, ilisema Sh milioni 132 zimeshatumika na wakati huo huo Sh
milioni 540 zimetengwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa dengue
ulioibuka jijini Dar es Salaam.
Serikali kupitia
kwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Stephen Kebwe katika
taarifa yake bungeni, ilisema imeshafanya utafiti mkoani Kagera, Morogoro
na Kigoma na kuthibitisha kuwa haijaathirika na ugonjwa huo.
Dk
Kebwe alisema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukabili ugonjwa huo
kadri itakavyohitajika. Alihimiza uvaaji wa nguo ndefu na zenye mikono mirefu
hususani katika maeneo ambayo ugonjwa huu umeripotiwa kuepuka kuumwa na mbu
husika.

No comments:
Post a Comment