Baba mzazi pamoja na walezi wa mtoto
anayedaiwa kufichwa kwenye boksi kwa takribani miaka mitatu, wamefikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini
Morogoro na kusomewa mashitaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto
huyo.
Rashid Mvungi (47), mkazi wa Lukobe na mtumishi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Morogoro, ambaye ni baba wa mtoto huyo pamoja na wanandoa Mariamu
Said (38) na mumewe, Mtonga Omar (30) walifikishwa mahakamani jana.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo, Wakili wa
Serikali, Sunday Hyera kwa kushirikiana na Mwendesha Mashitaka wa polisi,
Anganile Msiani walidai washitakiwa
walitenda makosa hayo kati ya Desemba mwaka 2010 na Mei mwaka huu katika eneo
la Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Walidai katika kipindi hicho, washitakiwa
wakiwa walezi wa mtoto huyo, walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi
akiwa ndani ya boksi na hivyo kumsababishia magonjwa.
Walitaja maradhi yaliyomkumba mtoto huyo
akiwa ndani ya boksi pamoja na utapiamlo, maumivu ya kifua na mvunjiko wa
mifupa katika maeneo ya mikono na miguu.
Mawakili hao walidai upelelezi wa kesi hiyo
umekamilika na kuiomba mahakama kutaja tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Wakili wa Serikali, Hyera alidai mahakamani
kwamba upande wa Jamhuri hauna kipingamizi kuhusu dhamana kwa washtakiwa.
Hakimu
Moyo alisema dhamana kwa washitakiwa iko wazi ,lakini kwa masharti ya
kila mmoja kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni tano kila
mmoja.
Alisema sharti lingine ni kwa wadhamini kuwa
na barua kutoka kwa waajiri wa kuaminika au serikali za mitaa.
Washtakiwa walishindwa kutimiza masharti
hayo, hatua iliyowafanya warejeshwe rumande.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 9 mwaka huu
kwa ajili ya usikilizaji wa awali.

No comments:
Post a Comment