Tuesday, April 8, 2014

SERIKALI MBILI KWA KURA THELUTHI MBILI BUNGENI INAWEZEKANA...

Wajumbe wakiinua mikono kukubaliana na moja ya hoja bungeni.
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kama wataacha ushabiki wa vyama na kujikita zaidi kwenye hoja, uwezekano wa kupatikana kwa theluthi mbili kuelekea katika mfumo wa serikali mbili upo.

Hayo yamethibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba 9 ya Bunge Maalumu la Katiba, William Ngeleja  wakati akizungumza na mwandishi jana.
Ngeleja alisema kwamba katika kamati yake wajumbe waliacha ushabiki na kujikita katika hoja na wakati wa kura, theluthi mbili zilipatikana bila dhiki.
Ngeleja alisema kwamba kamati yao imepata theluthi mbili kwa sura zote mbili-ya kwanza na ya sita walizojadili.
Sura ya kwanza inazungumzia jina la nchi, mipaka, alama, lugha na tunu za taifa wakati ile ya sita inazungumzia muundo wa Muungano wa Tanzania.
Kwa taarifa hiyo, Ngeleja amewavunja nguvu wanaodai kuwa tathimini inaonesha mambo yatakuwa magumu .
Miongoni mwa waliokaririwa wakisema mambo yatakuwa magumu ni Jussa Ladhu, ambaye pia ni  Mjumbe wa Bunge Maalumu.
Mwakilishi huyo wa Mji Mkongwe kupitia Chama cha Wananchi (CUF), amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuna kukosekana kwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar katika kupitisha baadhi ya ibara katika sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012 sheria Na. 26 (2) ya sheria, ambayo inasema ili katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge Maalumu itahitaji kupitishwa na theluthi mbili ya wajumbe wa kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu ni 639 ambapo Tanzania Bara watakuwa ni 415 sawa na asilimia 65 wakati wa Zanzibar ni 224 sawa na asilimia 35.
Kamati 12 zimeundwa kila moja ikiwa na wajumbe 52; ambao kati yao, 34 ni kutoka Tanzania Bara na 18 ni wa Zanzibar.
Ngeleja alisema, “kwa sura zote na kwa ibara moja baada ya nyingine tumefanikiwa kupata ushindi wa theluthi mbili ni kwa asilimia mia moja.
Hii maana yake nini? Maana yake ni kuwa kwenye bunge la Katiba theluthi mbili inawezekana.”
Alisema sababu za kupata theluthi hizo ni kwa wajumbe kujielekeza kwenye hoja badala ya ushabiki wa kisiasa au itikadi ya chama fulani.
“Kamati yetu watu walikuwa wanashindana kwa hoja,” alisema. Alisema ndani ya kamati hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Kidawa Salehe, waliokuwa wanashabikia mfumo wa serikali tatu walishindwa kushawishi namna ambavyo mfumo huo utafanikiwa wakati nchi washiriki wa muungano hawana mamlaka kamili ya dola.
“Tanganyika haipo, Zanzibar yenyewe haina mamlaka kamili ya dola. Sasa hapo uthibitisho wa serikali tatu unatoka wapi?,” alihoji Ngeleja na kuongeza: “Kukosekana kwa mamlaka kamili kwa pande zote mbili za muungano ni pigo kwa wanaoshabikia shirikisho la serikali tu.”
Alisema  ibara ya 1 (3) ya Rasimu ya Katiba inachambua muundo wa muungano na inapendekeza kuwepo kwa shirikisho.
“Lakini wanasahau kuwa shirikisho ni hati ya makubaliano ya muungano.”
“Ushabiki huo unaleta mgongano mkubwa kutokana na dhamira ya watu. Hati ya muungano inaelekeza muundo wa serikali mbili na si vinginevyo. Rasimu inapoelekeza shirikisho ni mwendelezo wa muungano, ni udhaifu wa hoja,” alifafanua.
Alisema hoja ya mfumo wa shirikisho ya serikali tatu itaibua hamasa kwa wananchi wa pande zote kudai uraia wa nchi zao, jambo ambalo kwa mujibu wake,  litasababisha mgogoro mkubwa baina ya Watanzania.
“Unajua, muungano huu ni wa watu si wa viongozi wala watawala. Watu wameungana kwa uraia wao wa Tanzania, sasa kudai shirikisho ni kujirudisha nyuma,” alisema Ngeleja.
Mjadala wa wazi kuhusu sura mbili za rasimu ya Katiba zenye maudhui muhimu kuhusu Muungano unafanyika wiki hii baada ya Bunge Maalumu la Katiba kumaliza kupitia sura hizo.
Kamati karibu zote zimeshamaliza kujadili na kuamua kwa kura kuhusu sura ya Kwanza na ya Sita. 
Akiahirisha Bunge Maalumu Ijumaa iliyopita, Makamu Mwenyekiti, Samiah Suluhu, alisema kesho Kamati ya Uandishi itakutana na kuandika taarifa ya kila Kamati.
Baada ya kumaliza kazi hizo, Samiah alisema keshokutwa, wenyeviti 12 wa kamati za Bunge Maalumu, watatakiwa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi ya  Katibu wa Bunge hilo.
Bunge hilo Maalumu linatarajiwa kuitwa tena Alhamisi. Pamoja na mambo mengine, kila Mwenyekiti wa Kamati, atawasilisha taarifa yake na baada ya hapo ndipo mjadala kuhusu sura hizo ambao uliokuwa siri katika Kamati hizo, utakuwa wazi.
Baadhi ya wenyeviti wa Kamati waliozungumza na waandishi wa habari walielezea kushindwa kufikia masharti ya theluthi mbili au zaidi ya kura ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na hivyo hivyo kwa wanaotoka Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati Namba 10, Anna Abdallah, alisema katika baadhi ya ibara za Sura ya Kwanza na Sura ya Sita, walishindwa kupata kura zinazokidhi masharti ya Kanuni za Bunge Maalumu na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. 
“Kwa bahati mbaya wajumbe wa Zanzibar wako 15, sasa ili kupata theluthi mbili, tunapaswa kupata kura kumi na Tanzania Bara tupo 35, ili kupata theluthi mbili tunapaswa kupata kura 23.
“Sasa ibara nyingi tulizopiga kura, hatupati theluthi mbili, tulipofikia katika masuala ya serikali tatu au mbili, wengi walisema serikali mbili na kila mtu alitoa sababu zake na wachache walisema shirikisho,” alisema.
Alisema kwa upande wa Tanzania Bara katika suala la muundo wa Muungano, theluthi mbili ilipatikana lakini kwa Zanzibar haikupatikana.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu, alisema katika kamati anayoiongoza, walipata changamoto hiyo ya kukosa theluthi mbili ya kura.
“Katika Ibara ya kwanza tu, tulipopiga kura matokeo yalipotoka, hatukupata theluthi mbili kutoka Zanzibar wala Tanzania Bara,” alisema Ummy.
Katika mjadala huo pia, waliotaka neno shirikisho liondolewe walikuwa na hoja ya serikali mbili na waliotaka lisiondolewe ni wajumbe waliokuwa na hoja ya serikali tatu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed, alisema hata katika Kamati hiyo, hawakupata theluthi mbili ya kura kutoka kila upande wa Muungano katika baadhi ya ibara.
Alitoa mfano wa Ibara ya Kwanza ya Sura ya Kwanza kuhusu Tanzania ni Shirikisho, ambapo wengi walitetea ibaki kama ilivyo, lakini Zanzibar hawakupata theluthi mbili ya kura.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, alisema katika kamati hizo kuna idadi ndogo ya wajumbe ambayo inasababisha upatikanaji wa theluthi mbili ya kura kuwa mgumu.
“Theluthi mbili ina ugumu, kwa mfano hapa kwetu wajumbe kutoka Zanzibar wapo 19, ili upate theluthi mbili unapaswa kupata kura 13, sasa unaweza kupata 12 na saba zikakataa, hapo umekosa mjumbe mmoja tu kupata theluthi mbili.  
“Nadhani hili la theluthi mbili, tuliangalie kwa watu wengi kule kwenye ukumbi mkubwa (bungeni),” alisema Profea Mbarawa.

No comments: