![]() |
| Anne Makinda. |
Aliyasema hayo jana wakati akitoa salamu za wabunge na viongozi wa siasa kwenye ibada ya kumuombea aliyekuwa Askofu wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Dodoma, Godfrey Mhogolo ambaye alizikwa jana kwenye viwanja vya kanisa hilo mjini hapa.
Makinda alisema kama kila mmoja anaipenda Tanzania, basi analazimika kufanya maombi.
"Tunaomba sala zenu kama nchi itasambatarika, katiba inaweza kuwa chanzo mtuombee, kama mnaipenda nchi hii iendelee kuwa na amani, mtuombee," alisema.
Alisema enzi za uhai wa Askofu Mhogolo, alikuwa ni rafiki wa kila mtu na alipokea kwa mshtuko mkubwa habari za kifo chake.
"Niliposikia kwa mara ya kwanza sikuamini, lakini kule mjengoni nikakaa na Askofu mstaafu Donald Mtetemela nikamuuliza je habari nilizosikia ni kweli akasema ni za kweli, nimeshtushwa sana na kifo hiki," alisema.
Alisema Mungu amempenda zaidi Askofu Mhogolo kilichobaki ni kumuombea apumzike kwa amani.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya aliahidi kanisa litafanya kazi ya kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili suala la kutafuta katiba lifanyike salama.
Alisema ni wakati wa kuiombea serikali katika kipindi hiki kigumu cha utengenezaji wa Katiba mpya.
"Tuko hapa kwa vile nchi ina amani lakini tungekuwa nchi ya vita watu wangekuwa wanaondoka hapa kwa kujificha, tuna wajibu wa kuombea nchi ili iwe na amani ma kuliombea Bunge la Katiba ili makusudi ya Mungu yatimie," alisema.
Alisema Mungu ametupa Watanzania fursa ya kutengeneza Katiba mpya ambayo itakuwepo kizazi na kizazi na kutaka wabunge wa Bunge Maalumu kutumia vizuri nafasi hiyo adimu ambayo wanaweza wasiipate tena.
Kauli ya Makinda na Askofu Chimeledya imekuja wakati wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa Dodoma kuijadili rasimu ya pili ya katiba mpya, lakini licha ya kuwapo mjini humo kwa zaidi ya siku 40, mjadala rasmi haujaanza huku mvutano ukiendelea katika kanuni zitakazoongoza mchakato huo.
Awali suala la kanuni na mjadala wa rasimu hiyo mpya ulitarajiwa kufanyika kwa siku 70 na zingeweza kufika hadi siku 90 kwa kibali maalumu cha Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, kutokana na jinsi mambo yalivyo hadi sasa ndani ya bunge hilo, wachambuzi wa mambo wanatabiri kuwa huenda dhamira njema ya Serikali itaendelea kupata majaribu kutokana na mchakato huo kutokwenda kwa ratiba iliyotarajiwa awali.
Wakati mambo yakiwa hivyo ndani ya Bunge, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe amesisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu hiyo na kwamba Katiba bora ipatikane kwa maridhiano badala ya mivutano na kutunishiana misuli.
Aliyasema hayo jana wakati wa kongamano la wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi Nje ya Bunge Maalumu la Katiba (Ukawa-nje) lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Katika kongamano hilo, Mbambabe alisema; "Ukawa nje ya bunge tunasisitiza kwamba katiba bora itapatikana kwa maridhiano na siyo mivutano na kutunishiana misuli, kwa mtindo huo haitapatikana."
Aidha, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Shaweji Mketo alisema, Ukawa-nje wako tayari kutumia gharama zozote ili kuhakikisha Katiba ya Watanzania inapatikana.
Alisema kama kuna mtu anadhani katiba itakayopatikana itakuwa kwa manufaa ya chama cha siasa au mtu mmoja atakuwa anajidanganya kwani lengo ni kuwa na katiba yenye maslahi kwa wote.
"Tupate Katiba itakayokuwa na maslahi ya wakulima, wafugaji, wafanyakazi na watu wengine wote bila kujali utofauti wao," alisema Mketo.
Naye kiongozi wa Ukawa-Nje ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Dk Willibrod Slaa aliwataka wabunge wa bunge hilo kujadili rasimu iliyopo badala ya kujadili vitu ambavyo havipo, kwani watakuwa wanapoteza muda.
Aidha, alisisitiza kuwa suala la Ukawa-nje kuzunguka nchi nzima kwa ajili kuwafahamisha Watanzania liko palepale.
Alisema inatakiwa ieleweke kuwa katiba inayotengenezwa si kwa ajili ya chama au mtu binafsi bali ni kwa ajili ya maslahi ya wananchi wote.
Vyama vya upinzani vyenye wajumbe kwenye Bunge Maalumu la Katiba waliunda Ukawa wakati bunge hilo linaanza vikao vyake Februari na tangu wakati huo umekuwa ukipinga na kutoa kasoro kadhaa katika uendeshaji wa bunge hilo tangu kuanza kwa kazi ya kutengeneza kanuni hadi kamati za kuchambua rasimu zilipoanza kazi.
Mbali na Ukawa kuwepo bungeni, wiki iliyopita vyama hivyo vya upinzani vikaunda Ukawa-nje kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko na kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na mambo kadhaa yanayoendelea bungeni kwenye safari ya kupatikana katiba mpya ikiwemo kufanya mikutano nchi nzima.

1 comment:
hivi huyu mama ana akili kweli, watu wanakula posho ya serikali harafu wanafanya madudu na kurumbana tu badala ya kufanya kilichowapeleka humo bungeni, harafu huyu spika analeta mambo ya hekaya za abunuasi eti kila mtu awaombee, kama wameshindwa kazi fukuza wote na vunja hilo bunge...kwa kweli hawa viongozi wetu wameoza!!!
Post a Comment