![]() |
| Baadhi ya wakazi wa kisiwa cha Pemba wakiwa katika shughuli zao za kila siku. |
Hayo yamo katika taarifa ya mtandao huo iliyolenga kupongeza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kwenye Bunge la Katiba Maalumu, na kusainiwa na Mwenyekiti wake, Shehe Haji Faki.
Umesema chokochoko haziwezi kuwa na msingi wowote kwa Wazanzibari na Wabara, bali zinahatarisha usalama.
Akizungumzia manufaa ya Muungano uliopo, Faki alisema siyo tu kwenye masuala ya ongezeko la ajira serikalini, bali pia kibiashara, Wazanzibari hususani wao wanaotoka Pemba wamepiga hatua kubwa kwa kufanikiwa kukuza mtaji wao hadi kufikia Sh trilioni 1.2.
"Kuwepo kwa dalili zozote za kuvunjika muungano hakuwezi kutuacha salama sisi Wapemba tuishio huku Bara. Chokochoko zote na ishara mbaya za chuki kati ya Wabara na Wazanzibari, hazitaweza kuimarisha msingi mkubwa wa Muungano uliojengwa kwa muda mrefu na waasisi wetu," alisema Faki.
Aliongeza kuwa uwepo wa muungano umewafaidisha na unaendelea kuwafaidisha kwa sababu wameweza kuoana na watu wa bara, hivyo kuendeleza undugu.
"Pamoja na kuoana, Wapemba tuishio bara tumeweza kushiriki katika shughuli za kilimo na ufugaji na hivyo kuongeza tija katika sekta hiyo", alisisitiza.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa mtandao, idadi ya Wapemba wanaoishi Bara imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kufikia watu zaidi ya 800,000 mwaka 2012.
Katika hatua nyingine, NEPPELTA imempongeza Rais Kikwete kwa hotuba yake ikitajwa ni yenye busara, hekima na upole. Mtandao huo umeeleza kufarijika kusikia Rais akikemea serikali tatu kwa sababu zinatishia uwepo wa muungano.
"Tumefarijika kwa sababu Rais amekemea serikali tatu kwa kutaja udhaifu wa kila moja, pamoja na kutoa hoja za msingi kuhusu athari zake kwa muungano," alisema.
Faki alifafanua kuwa dhima ya muungano huo ni historia ya vizazi vya nchi hizo mbili zenye asili na historia zinazofanana ambazo wakoloni walizivuruga.
Wanamtandao hao wamemhakikishia Rais Jakaya Kikwete kumuunga mkono katika jitihada zake za kulinda muungano kwa kupambana na wenye nia ya kuuvunja, kwa kutumia itikadi za dini na siasa.
Alisisitiza muungano unastahili kuimarishwa kwa sababu una faida na maslahi kwa wananchi wa nchi washirika.
Alisema mpango wa kuunganisha Zanzibar na Tanganyika ulioanza mwaka 1963, ulikuwa ni utashi wa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume na ulilenga kuleta maslahi mema kwa wananchi.
Hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba, iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete Ijumaa iliyopita, na hotuba ya Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, sasa hazitajadiliwa katika Bunge Maalumu.
Uamuzi huo ulitangazwa jana asubuhi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ambaye alifafanua kuwa kuruhusu hotuba hizo kujadiliwa, kutavuruga utaratibu waliojiwekea wa kujadili Rasimu ya Katiba mpya.
Utaratibu wa kujadili Rasimu hiyo ni kwa Bunge Maalumu kujadili sura mbili mbili za Katiba, au kama Kamati ya Kanuni itaamua vinginevyo, zitajadiliwa sura tatu tatu ili kuendana na muda finyu uliobakia.
Sitta alisema ingawa alikubaliana na watoa hoja kuwa hotuba hizo zijadiliwe, lakini baada ya mashauriano, ilionekana fursa hiyo itatumiwa na wajumbe kujadili rasimu katika sura yoyote inayowagusa na kuharibu utaratibu huo uliopangwa.
Katika hotuba ya Rais Kikwete, pamoja na mambo mengine alizungumzia umuhimu wa muundo wa Muungano wa serikali mbili katika kulinda umoja, mshikamano na amani ya Watanzania.
Rais Kikwete aliweka wazi kuwa serikali ya tatu inayopendekezwa na Rasimu ya Katiba, hasa serikali ya shirikisho, haitakuwa na rasilimali na itakuwa dhaifu na kujikuta ikigeuka ombaomba kwa serikali za nchi wanachama na kutegemea hisani za nchi hizo kujiendesha.
Mbali na hoja hiyo, Rais Kikwete pia katika kuchambua takwimu za taarifa ya Tume, alisema wananchi wengi katika maoni hawakuzungumzia Muungano, jambo linaloonesha kuwa Muungano si kero kama unavyoelezwa na Tume.
Alibainisha kuwa katika sehemu hiyo ndogo ya Watanzania waliozungumzia Muungano, wengi ndio wamependekeza wa serikali tatu, ambao ndio waliotafsiriwa kuwa maoni ya wananchi wengi suala ambalo watetezi wa serikali mbili wanahoji kwa nini wachukuliwe kuwa ni maoni ya Watanzania wengi.
Aidha, Rais Kikwete alisema hata Sensa ya Watu Makazi, imebainisha kuwa karibu asilimia 90 ya Watanzania walioko, wamezaliwa baada ya 1964, hivyo hawajui hiyo Tanganyika inayopigiwa kampeni ifufuliwe.
Katika hotuba ya Warioba alisisitiza Muungano wa serikali tatu, akisema pamoja na mambo mengine kuwa Muungano wa serikali mbili ulioachwa na waasisi wa Muungano ulikuwa wa nchi moja, lakini kwa kuwa sasa ziko nchi mbili. Alisema Muungano wa serikali tatu ndio muafaka.

No comments:
Post a Comment