| Eva Kleruu (kushoto) na Amani Mwamwindi. |
Eva Kleruu (56) ambaye ni mtoto wa kwanza wa marehemu Dk Kleruu, alishindwa kuzuia machozi wakati akizungumza baada ya kukutana na Meya wa Manispaa ya Iringa, Amani (63), ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mwamwindi.
Dk Kleruu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani Desemba 25, 1971 na Mwamwindi aliyekuwa mkulima maarufu wa mahindi katika kijiji cha Isimani wilayani Iringa.
Tangu kifo hicho kitokee, miaka 43 iliyopita, kabla ya wanafamilia hao kukutana mwishoni mwa wiki, ilielezwa familia hizo hazikuwahi kukutana.
Katika mkutano huo ulioitwa ni wa maridhiano, uliofanyika katika ofisi ya Meya wa Manispaa ya Iringa, mwishoni mwa wiki, akizungumza huku akitokwa machozi, Eva alisema tukio hilo (la mauaji) lilikuwa likifanya familia ya Dk Kleruu, iogope kwenda Iringa.
Eva ambaye aliongozana na mumewe, alisema; “tumekuwa tukikumbuka historia ya maisha yetu na jinsi marehemu baba yetu alivyouawa.”
Huku akitetemeka na kutokwa machozi, Eva alisema “Pamoja na hofu hiyo, niliweka nadhiri kwamba ipo siku nitafika Iringa na kutembelea sehemu ambayo marehemu baba yangu aliuawa katika shamba la Mwamwindi.”
Alisema baada ya kutembelea eneo hilo, alipanga kukutana na watoto wa mkulima Mwamwindi, kuweka maridhiano yatakayofanya watumie tukio hilo la mauaji ya baba yao, kuungana.
Kwa kupitia Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga, Eva alisema waliweza kukutana na kufanikisha azma hiyo.
“Ile siku imefika na leo nimekutana na mtoto wa kwanza wa Said Mwamwindi, Meya Amani Mwamwindi na kumaliza tofauti zetu zilizosababishwa na mauaji hayo,” alisema Eva.
Alisema baada ya kukutana na Meya Mwamwindi na kuweka kando tofauti za kihistoriaa baina ya familia zao, anajihisi atakuwa sehemu ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa.
Alisema kwa kupitia Kampuni yao ya Power Supply Cooperation, wako tayari kuhakikisha kwamba miradi midogo ya uzalishaji umeme, inajengwa katika maeneo mbalimbali mkoani Iringa kufikisha kwa watu wengi zaidi.
Katika kikao chao hicho, ambacho pia Meya Mwamwindi alitokwa machozi, walikubaliana kukutana na familia zao na kutoa taarifa ya maridhiano hayo.
Kwa upande wake, Meya Mwamwindi alisema, “Nimefurahishwa kukutana na dada yangu huyu na kuondoa tofauti zetu za kihistoria.”
Mwamwindi alisema; “kabla na baada ya tukio hilo litokee miaka 43 iliyopita, familia zetu zilikuwa hazijuani vizuri. Na sisi tulikuwa watoto, leo tunakutana tukiwa watu wazima, ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu.”
Walisema baada ya kikao hicho, kilichohudhuriwa na baadhi ya ndugu, watapanga siku nyingine, ambayo kwa pamoja, familia hizo mbili zitakutana zikiwa na wawakilishi wengi zaidi.
No comments:
Post a Comment