Wednesday, March 19, 2014

WANANCHI WA ZANZIBAR WAKATAA MUUNDO WA SERIKALI TATU...

Sehemu ya mji wa Unguja.
Asilimia 60 ya wananchi wa visiwani Zanzibar waliotoa maoni yao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wametaka muundo wa Muungano wa serikali ya mkataba na hakuna hata mwananchi mmoja aliyetaka muundo wa serikali tatu.

Kwa upande wa Tanzania Bara asilimia 61 walitaka muundo wa serikali tatu, na hakuna aliyependekeza muundo wa serikali ya mkataba.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Jaji mstaafu Joseph Warioba, wakati anawasilisha maoni ya wananchi na taasisi mbalimbali yaliyokusanywa na Tume yake kwa Bunge Maalum la Katiba, alisema karibu wananchi wote waliotoa maoni kwa upande wa Zanzibar walijikita kuhusu Muungano.
“Kati ya wananchi karibu 38,000 waliotoa maoni kuhusu Muungano, wananchi 19,000 Zanzibar walitoa maoni kuhusu muundo wa Muungano. Asilimia 34 walipendekeza serikali mbili, asilimia 60 muungano wa mkataba na wananchi 25 sawa na asilimia 0.01 walipendekeza serikali moja,” alifafanua Jaji Warioba.
Jaji Warioba alisema taasisi nyingi kama vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuiya za kidini zilipendekeza muundo wa serikali tatu.
Alisema kwa upande wa Tanzania Bara, wananchi wengi waliotoa maoni kuhusu Muungano walijikita kwenye Muundo wake kama njia ya kuondoa kero ambapo zaidi ya wananchi 39,000, walitoa maoni kuhusu Muungano na kati ya hao karibu 27,000 walizungumzia muundo.
Alisema asilimia 13 walipendelea serikali moja kwa Tanzania Bara huku asilimia 24 wakitaka serikali mbili na asilimia 61 serikali tatu.
“Suala la muundo wa serikali tatu limechukua nafasi kubwa sana katika mjadala tangu Tume ilipozindua Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Mjadala wa muundo wa Muungano umekuwa mkubwa kwa kiasi cha kufunika mapendekezo mengine yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema.
Jaji Warioba alisema Tume yake iliamini Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika kifungu cha 9(2) iliyotoa mwongozo wa kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama na Serikali ya Mapinduzi ulikuwa mwongozo wa Tume yake na si kwa wananchi.
“Tume iliamini sheria haikukusudia kuwazuia wananchi kutoa mawazo yao kwa uhuru bila ya kizuizi wala mipaka hivyo ilipokea mawazo ya kila aina,” alisema.
Alisema Tume ilifuata njia ya wananchi kuwa huru katika  kutoa maoni yao kwa kuwaruhusu kusema chochote kuhusu maeneo yao, ikiwa ni pamoja na suala la Muungano na kutowapa muongozo kama kujibu maswali kwa njia ya madodoso.
Warioba ameeleza kwamba taasisi za Serikali zilizowasilisha mapendekezo yao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu  Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais, zimependekeza mfumo wa serikali tatu.
Alilitaja Baraza la Wawakilishi na kueleza kuwa lilipendekeza kuwepo mamlaka huru ya Zanzibar, Tanganyika  na mamlaka ya Muungano na kutaka iwekwe wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya mamlaka.
Alitaja Baraza la Ofisi ya Waziri Mkuu, ambalo lilipendekeza kuhusu uongozi wa Taifa kwa kutaka kuwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu wa Serikali ya Tanganyika na Waziri Mkuu wa Serikali ya Zanzibar.
Katika mapendekezo yao Ofisi wa Waziri Mkuu, Warioba alisema walieleza ni kwa sababu hakuna umuhimu wa kuwa na marais watatu katika nchi moja na wala neno rais halimuongezei  hadhi kiongozi yeyote.
Mapendekezo yao pia yalitaka mawaziri wakuu hao wapewe nafasi kuwa watendaji zaidi na hivyo kusimamia serikali za washirika.
“Ofisi ya Makamu wa Rais, ilipendekeza kuwe na Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na wakuu wa serikali za washirika wa Muungano wapewe vyeo vingine, vinavyoendana na hadhi na mamlaka zao. Pia katika kutaja hizo serikali tatu inabidi zitenganishwe ili serikali ya Muungano ionekane ndiyo ya juu,” alisema Warioba.
Mbali na hao, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipendekeza kuwepo kwa Tume ya Utumishi wa Bunge, ambayo inajumuisha wajumbe, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano(Mwenyekiti), Spika wa Bunge la Tanzania Bara na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

No comments: